MWENYEKITI wa Utume na Uinjilisti wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Julias Lugendo akizungumza na wanahabari hawapo pichani.
Baadhi ya viongozi wa Kanisa la Anglikana wakiongoza sala.
Askofu wa kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Ruaha, Joseph Mgomi akitoa Sala.
…….
NA DENIS MLOWE, IRINGA
MWENYEKITI wa Utume na Uinjilisti wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Julias Lugendo amesema mwenendo na ufuatiliaji wa karibu na utatuzi wa changamoto mbalimbali yanayojitokeza nchini unaofanywa na Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni wa kuridhisha na kuungwa mkono na umma kwa maslahi mapana ya nchi.
Akizungumza na wanahabari wakati wa Kongamano la Wainjilisti na Makatekisti wa Anglikana wote wa Kanisa hilo Tanzania kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Kishirikishi Cha Mkwawa, Askofu Lugendo alisema jamii inapita katika nyakati ngumu ambazo zimejaa uharibifu kila namna na maadili yamepotea na sio kwa walioko ulaya Bali hata kwenye taifa la Tanzania.
Askofu Lugendo alisema serikali ya awamu hii imejipambanua katika kutatua changamoto za jamii na hii ni kutokana na jamii kuwa tulivu yenye amani inayotokana na mafundisho wanayoyapa makanisani Hali ambayo imekuwa kazi nyepesi kwa nchi kuwa tulivu na Serikali kuweza kufanya kazi na maendeleo kuonekana.
Alisema kuwa taifa la Tanzania liko katika amani , milango ya kibiashara imefunguliwa na kama Kuna madogo na makosa madogo madogo yanajitokeza ni jambo la kawaida ambayo yanataturika kwa umakini na Serikali .
Akielezea mmomonyoko wa maadili,Askofu Lugendo alisema jamii ya sasa baadhi ya watu wamemkacha Mungu na kufanya mambo yasiyompendeza Ikiwemo baadhi ya maaskofu katika makanisa mengine kuhubiri Yale ambayo hayako kwenye Biblia na kuwadanyanya waumini wafungue pochi watapata Hela bila kuwekeza popote.
*Hali hii imeendelea kujitokeza kwa baadhi ya viongozi wa dini kuwadanganya wauminii Hali ambayo haimpendezi Mungu na kuwataka kubadilika na kufanya mahubiri mema.”alisema
Aliongeza kuwa endapo kila kiongozi wa dini akifanya mahubiri mema basi jamii itakuwa njema na nchi itakuwa njema na yenye amani na utulivu
Amewataka wainjilisti na makatekista kutumia kongamano Hilo kujifunza na kupeleka injili kuanzia ngazi ya chini kabisa kuweza kupata jamii yenye upendo mkubwa, amani na utulivu.
Alisema jumla ya dayosisi 28 zimefika kwenye kongamano Hilo la siku sita kuanzia Septemba 19 Hadi Septemba 24.kutoka mikoa yote nchini ikiwa na lengo la kukaa pamoja, kushauriana na kupeana elimu ambayo itasaidia kanisa la Anglikana nchini kuwa na lugha Moja.
Kwa Upande wake Askofu Mwenyeji wa kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Ruaha, Joseph Mgomi amewataka waumini wa kanisa hilo kujiepusha na imani zenye mmomonyoko wa maadili na na kuondokana na kuiga Yale ambayo hayampendezi Mungu.
Askofu huyo alisema sifa Kubwa ya mtumishi wa Mungu ni uaminifu, upendo , staha na ushirikiano kwenye jamii ila wapo baadhi ya Watu ambao wanajivisha vyeo vya kila aina Ili kuwavuta waumini kwa maslahi yao jambo ambalo si sawa.
Alisema kuwa suala la mmomonyoko wa maadili kwa jamii limeendelea kuchochewa na imani potofu na Sasa wapo ambao wanahamasisha Ndoa za jinsia Moja na Mambo mengine yasio faa kwenye jamii hivyo kama Wainjilisti kukemea vikali kwenye jamii wanazoishi.
“Wajibu wa wainjilisti na makatekista watumishi wa kweli wa kanisa kupinga mafundisho yote yasiyo faa kwenye ambayo sio ya kweli” Alisema