Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka Mwanakwerekwe Zanzibar watembelea Chuo kikuu Mzumbe Kampasi Kuu. Ugeni huo umetembelea Chuoni hapa leo tarehe 19/09/2023.
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko, Bi. Lulu Mussa (Katikati), Afisa Masoko Bi. Ester Kiondo (wa pili kulia), Afisa Rasilimali Watu, Bi. Rahma Mziray (wa pili kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo Cha Miliki, Bw. Wolta Shiyo (kulia), wakiwa na wageni kutoka Mwanakwerekwe Zanzibar walipotembelea Chuo Kikuu Mzumbe leo tarehe 19/09/2023.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Mipango,Fedha na Utawala), Prof. Allen Mushi akiwaelezea wageni toka Zanzibar shughuli za kitaaluma na kijamii zinazotekelezwa na Chuo kikuu Mzumbe mapema leo tarehe 19/09/2023
Afisa Rasilimali Watu, Bi. Rahma Mziray wa pili kushoto akiwaonesha wageni kutoka Zanzibar miundombinu ya Chuo Kikuu Mzumbe.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa CCM Tawi la Mwanakwerekwe Zanzibar, walipotembelea Chuo Kikuu Mzumbe leo tarehe 19/09/2023.
………..
Katika mwendelezo wa kudumisha mahusiano na jamii, Chuo Kikuu Mzumbe kimepokea wageni ambao ni Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mwanakwerekwe Zanzibar. Wageni hawa wamefika Mkoani Morogoro kwa ziara ya kichama na moja ya eneo ambalo wametembelea ni Chuo Kikuu Mzumbe.
Akizungumza mapema baada ya kuwapokea wageni hao tarehe 19 Septemba, 2023, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo ambae ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, amewakaribisha na kuwaeleza historia fupi ya Chuo Kikuu Mzumbe tangu kuanzishwa kwake, pia ameeleza juu ya huduma za kitaaluma na kijamii zinazotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe.
Prof. Mushi ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kukifanya Chuo Kikuu Mzumbe kuwa tunu ya Taifa kwa kukisaidia kuboresha miundombinu yake na hasa kwa wakati huu kwa kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi “HEET – Project”, mradi unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifunza ili kuzalisha wataalamu wataosaidia kukuza uchumi wa Taifa letu.
Aidha Prof. Mushi amewaeleza wageni hao kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinajivunia kuendelea kuwa tanuru la kuoka viongozi wengi na mahiri chini, huku akimtaja Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa miongoni mwa wanafunzi waliosoma iliyokuwa IDM – Mzumbe.
Ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea na kuona maeneo mbalimbali ya Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni pamoja na Maktaba, Majengo ya hosteli yaliyopewa majina ya waliowahi kuwa viongozi mashuhuri wa Tanzania na Afrika na hosteli ya Matola mahali ambapo Dkt. Samia Suluhu Hassan alikaa wakati anasoma iliyokuwa IDM – Mzumbe.
Pia wametembelea na kujionea baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la utawala, uwanja wa mahafali, hosteli na madarasa ambayo baadhi yamekwisha kamilika na yanatumika eneo la Maekani.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo Bw. Ramadhani Fatawi Issa, Mwenyekiti wa Tawi la Mwanakwerekwe na Mkuu wa msafara katika ziara hiyo, amekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa mapokezi mazuri na amepongeza namna ambavyo Chuo kinajipambanua katika kuboresha miundombinu ya elimu. Amesema wamefurahi kuona namna ambavyo historia za wasisi wa Taifa zinaenziwa na kuendelea kurithishwa kwa vizazi hadi vizazi.
“Tunashukuru sana kwa mapokezi mazuri, tumefurahi kupata wasaa wa kufika mahali hapa, tumejifunza mengi. Nasi sasa tunaporudi Zanzibar tutapeleka salamu na tutakuwa mabalozi wazuri wa Chuo Kikuu Mzumbe ili wanetu waje kusoma hapa.” Alisema Bw. Ramadhani Fatawi Issa.