Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Uwanja wa Mitwero mkoani Lindi tarehe 19 Septemba, 2023.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza jambo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Sophia Mjema, katika mkutano wa hadhara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Mitwero mkoani Lindi tarehe 19 Septemba, 2023.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiteta jambo na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, katika mkutano wa hadhara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Mitwero mkoani Lindi tarehe 19 Septemba, 2023.
Wananchi waliofika katika Uwanja wa Mitwero, mkoani Lindi wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, wakati akielezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo.
…….
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema shilingi bilioni 400 zitatumika katika ukarabati wa Barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi kupitia majadiliano yaliyofanywa kati ya Serikali na Benki ya Dunia (WB). Pia, ampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara inayounganisha vipande kutoka Masasi- Nachingwea – Liwale (km 175).
Waziri Bashungwa aliyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na wananchi uliofanyika katika Uwanja wa Mitwero mkoani Lindi wakati akitoa salamu na kueleza utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo mkoani humo.
Waziri Bashungwa alisema pamoja na Serikali kuendelea kutafuta fedha za ujenzi wa barabara hiyo lakini Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ameridhia kusainiwa kwa barabara hiyo.
“Rais Samia Suluhu Hassan umetuelekeza Wizara ya Ujenzi hata kabla fedha wakati tunaendelea kuzitafuta, umeelekeza kwa namna ambavyo unawajali wananchi wa mikoa hii miwili kwamba tusaini huku ukiendelea kupambana kutafuta fedha ya barabara hii ambayo italeta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara”, alisema Bashungwa.
Ameongeza kuwa Mhe. Rais ameelekeza mkandarasi wa barabara ya Nachingwea – Ruangwa – Nanganga yenye urefu wa kilometa 53.2 ambayo tayari ujenzi wake umefikia asilimia 41 aendelee na ujenzi wa barabara hiyo hadi Nachingwea ambapo itakuwa na jumla ya urefu wa kilometa 106.
Kuhusu Barabara ya Nangurukuru – Liwale (km 230) Waziri Bashungwa alisema tayari Serikali imetenga fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 72 kuanzia Liwale hadi Choya.
“Mhe. Rais kama hiyo haitoshi kipo kipande cha Barabara ya Ruangwa- Namichiga kilometa 20 ambacho kwa sasa kipo kwenye mipango ya kuwekwa lami kupitia mradi wa RISE, sasa ukiona mahaba na Watanzania wakijitokeza kwa wingi unakopita ni kwamba wewe ni Rais wa vitendo na wanaona kazi kubwa ya Serikali unayoiongoza”, alisema Bashungwa.