Utafiti wa Mradi wa EFLOWS waonesha maji yanapungua kwenye mito
Wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakiwa kwenye kikao cha mawasilisho ya Matokeo ya Utafiti wa miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya mto huo kilichoketi juzi wilayani humo.
………………………………………………
Na Calvin Gwabara, Mbarali.
Matokeo ya Utafiti wa miaka miwili
kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya Mto Mbarali Mkoani Mbeya yameonesha kuwa
Maji yanapungua na hii ni kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya matumizi
ya maji kuongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo vya maji vya mto huo.
Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet
Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye ni Mtafiti
Mkuu wa Mradi huo wa miaka miwili wa Utafiti
wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha
Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa
Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania
(EFLOWS) wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau wa maji wa mto
Mbarali wilayani humo Mkoani Mbeya.
“Tulichokiona kwenye utafiti ni kwamba
wingi wa maji kwenye mto unaendelea kupungua, wahitaji wa maji wanaongezeka
lakini pia mabadiliko ya tabia nchi nayo yameathiri kwa kiasi kikubwa
mtawanyiko wa maji na mvua kwenye maeneo haya na hivyo kupelekea maji kupungua
mtoni na athari zake hasi zikionekana kwenye mifumo ikolojia ya mto hasa wakati
wa kiangazi. Tumeona uwepo wa matumizi makubwa ya maji bila vibali kwa kutumia
pampu, na uzalishaji mkubwa wa mchanga wakati wa mvua kutokana na shughuli za
kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo milimani na kwenye mashamba” alisema Prof.
Kashaigili.
Aliongeza” Shughuli za kibinadamu
zinazofanyika Mbarali kwa maana ya makazi, kilimo, ufugaji, ufyatuaji wa
matofali kwenye vyanzo vya maji na mtoni, kilimo cha vinyungu, moto na shughuli
zingine za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji kwenye
mto, lakini uchukuaji wa maji kwenye mto ndio umeonekana kuongoza kwa athari
hasi”.
Prof. Kashaigili amesema changamoto hiyo
ya matumizi makubwa ya maji imepelekea mto kukauka kabisa maeneo ya chini
wakati maeneo ya juu ya mto na katikati ukifika unakuta maji mengi yanatiririka
ambayo hayafiki mwisho yanaishia njiani kutokana na watu kuyachepusha na
kuyachota kwaajili ya shughuli zao mbalimbali hususani kilimo ambacho
hakizingatii matumizi sahihi ya maji hayo.
“Kwa maana hii ni kwamba Mto Mbarali
hauchangii chochote kwenye Mto Ruaha Mkuu hasa wakati wa kiangazi kwenye maeneo
ya uhifadhi na hii maana yake ikolojia ya mto na uendelevu wake imeathirika na
hivyo kushindwa kufikia malengo makubwa ya Kidunia ya maendeleo endelevu na
yale ya kitaifa ya kuifadhi na kuilinda baonuai ya mto” alifafanua Mtafiti huyo
Mkuu Prof. Kashaigili.
Mtafiti huyo aliyebobea kwenye tafiti za Masuala ya maji na
Mazingira Duniani amesema pamoja na Utafiti kutoa matokeo hayo kwa wadau hao