Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA Dkt. Baghayo Saqware akiwasilisha ripoti ya mafanikio kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Leo Septemba 18,2023.
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA Dkt. Baghayo Saqware akisalimiana na Eric Anthony Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina wakati alipowasilisha ripoti ya mafanikio ya TIRA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Leo Septemba 18,2023.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Bw. Deodatus Balile akifafanua baadhi ya mambo katika mkutano huo.
………………………….
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeendelea na usimamizi mzuri wa shughuli mbalimbali za bima na maendeleo katika sekta za kiuchumi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 huku ikijipanga kwa mipango kabambe kuhakikisha inafanya vyema zaidi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yamebainishwa Leo Septemba 18, 2023 na Kamishna wa Mamlaka hiyo Dkt. Baghayo Saqware wakati akiwasilisha ripoti ya mafanikio ya TIRA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Dkt. Saqware amebainisha kuwa kutokana na usimamizi huo mzuri, Mamlaka hiyo imeendelea kuchangia gawio kwa serikali kutokana na shughuli mbalimbali inazozifanya ikiwemo usimamizi wa miradi na usajili mbalimbali wa bima ambapo mpaka sasa Mamlaka imefanikiwa kuanzisha na kusimamia miradi na shughuli mbalimbali ikiwemo Konsotia ya Bima ya Kilimo, ili kusaidia utekelezaji wa skimu ya bima ya Kilimo Tanzania kwa ufanisi lakini pia imeendelea kuchangia kwenye upatikanaji wa ajira kwa vijana ambapo hadi kufikia Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa Watanzania 4, 173.
“Sekta ya Bima imekua kwa wastani wa asilimia 12.8 kwa mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka mitano mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka Tsh. Bilioni 691.9 mwaka 2018 hadi kufikia takribani Trilion 1.2 mwaka 2022, Mchango wa Sekta ya Bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 0.56 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 1.68 kwa mwaka 2021, jambo hili limesaidia Mamlaka kuendelea kuongeza gawio serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 Mamlaka imeweza kulipa gawio kwa serikali la jumla ya Tsh. Bilioni 2.9,” amesema Dkt. Saqware.
Kamishna huyo amessema kuwa, kwa sasa Mamlaka hiyo inasimamia mradi wa TIRAMIS (TIRA Management Information System) na TIRA-ORS (TIRA Online Registration System) ambayo imerahisisha huduma za utumaji na upokeaji wa taarifa za kibima miongoni mwa wadau, usimamizi wa biashara ya bima nchini, pamoja na kuharakisha uchambuzi wa takwimu na utoaji wa taarifa, lakini pia imeendelea kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi.
“Mamlaka imeanzisha Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi iliyozinduliwa tarehe 16 Novemba 2022, Konsotia hiyo ina malengo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza siyo chini ya asilimia 45 ada zitokanazo na gesi na mafuta, kuongezeka kwa uwezo wa kiufundi wa ndani na utaalam katika uandikishaji wa vihatarishi vya bima ya nishati ya mafuta na gesi katika soko la bima, kuongezeka kwa uwezo wa kifedha kugharamia sekta ya nishati na kuongezeka kwa uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika sekta ya bima ya nishati ya mafuta na gesi.” Amefafanua Dkt. Saqware.
Aidha amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Mamlaka hiyo imefanikiwa kusajili leseni kwa watoa huduma mbalimbali wa Bima nchini ikiwemo, Kampuni tatu (3) za Bima Mtawanyo kwa ajili ya kubeba dhamana ya Kampuni ya Bima kulipa mafao na fidia, Kampuni 35 za Bima Mtawanyokibali cha Biashara nje ya nchi, Kampuni thelathini na tatu (33) za Bima katika kuhakikisha malipo ya mafao na fidia kwa mkata bima na kuwekeza tozo za bima (premiums).
Nyingine ni pamoja na Wataalamu watano (5) wa Ushauri wa BimaMtawanyo (Reinsurance Brokers), Wataalamu ishirini na wanne (24) wa Ushauri wa Bima Mtawanyo waliopewa kibali cha kufanya Biashara-Nje ya Nchi, Wataalamu mia moja (100) wa Ushauri wa Bima (Insurance Brokers), Mawakala mia tisa na Thelathini (930) wa Bima (Insurance Agencies), Benkiwakala (Bancassurance Agency) thelathini na mmoja (31), Wauza Bima Kidijitali (Insurance Digital Platform) tisa (9), Wakadiriaji Hasara arobaini na sita (46), Kampuni nne (4) za Takwimu Bima (Actuarial Firms), Wachunguzi Binafsi wanne (4) pamoja na Maafisa Wauza Bima mia moja (100).
Mamlaka hiyo imeendelea na mkakati wake wa uelimishaji umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya bima ili kuhakikisha kuwa inawafikia asilimia 80 ya watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya kumi na nane (18) ifikapo mwaka 2030, ambapo hadi mwezi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo, Wizara ya Nishati na Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi na Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Hata hivyo Mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025/2026 kwa kushirikiana na wadau wa Bima inaendelea na utekelezaji wa Mipango na mikakati ya Taifa ambayo ni pamoja na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa (FYDPII-2020-2025), kuanzisha na kutekeleza Mpango wa kitaifa wa Bima ya Kilimo (Tanzania Agriculture Insurance Scheme), kuunganisha mifumo ya kidigitali na Taasisi mbalimbali za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA, ZRA kwaajili ya kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la Bima na kufungua ofisi za Bima Mtawanyo za Kikanda.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imeanzishwa kwa Sheria ya Bima ya mwaka 2009 Sura Na. 394 ikiwa na majukumu ya kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima, kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la bima na kurekebisha sheria pamoja na kulinda haki za mteja wa bima.