Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini, Ramadhani Ng’anzi akisikiliza maelezo baada ya kutembelea chuo hicho jijini Arusha.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini, Ramadhani Ng’anzi akizungumza na wafanyakazi wa chuo hicho alipotembelea chuoni hapo.
Julieth Laizer ,Arusha .
Arusha. Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani limezifungia vyuo vya mafunzo ya udereva 124 kutokana na kukosa sifa ya kutoa elimu hiyo.
Mbali na hatua hiyo, pia limepanga kuzifutia lesseni ya uendeshaji wa mafunzo hayo ili kuanza mchakato upya wa maombi watakapokidhi vigezo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini, Ramadhani Ng’anzi alipokuwa akikagua chuo cha ufundi Arusha (ATC) kinachotoa mafunzo ya udereva.
Amesema kuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani wamebaini unatokana na uzembe wa madereva wanaotengenezwa na vyuo husika hivyo wameanza na ukaguzi wao kujihakikishia ubora wa elimu waayoitoa Kama unakidhi vigezo.
“Tuko hapa chuo cha ufundi Arusha, kwanza kutembelea eneo lao la mafunzo lakini pia waalim na vifaa vyao katika muendelezo wa kaguzi zinazoendelea na nchini na bahati nzuri wao wamekidhi vigezo kikubwa wawafuatilie mawakala wao waliopo mikoani kuepuka rungu hili”amesema.
Amesema kuwa katika kaguzi za mwezi agost wamefanikiwa kukagua vyuo 230 ambapo 124 vimekosa sifa na wamefungia ambapo wanatarajia kuvifutia kabisa lesseni.
“Vyuo 106 pekee ndio zenye sifa na vinaendelea na kazi ikiwemo wana Eneo la kutosha na vitendea kazi, vifaa lakini pia walimu, na baada ya vyuo tutaanza kufanya operesheni maalum ya kukagua lesseni na vyeti vya madereva na visivyo na sifa tutavifuta ili kuweka nidhamu ya tasnia hii nzima” amesema Ng’anzi.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo ufundi Arusha, (ATC), Mussa Chacha amesema kuwa wanayofuraha kutembelewa na ugeni huo sambamba na kupata sifa za kuendesha mafunzo ya udereva nchini.
“Chuo chetu kwa upande wa uhandisi wamagari tumeweka pia mafunzo ya udereva ambayo yanatolewa na mawakala wetu katika matawi yaliyoko mikoa mbali mbali nchini, ambapo tunasisitiza uweledi na ufanisi kazini kwa lengo la kutengeneza madereva bora watakaoingia sokoni na kupunguza ajali kwa watu wetu”amesema
Mmoja wa wanafunzi wa udereva chuoni hapo amesema kuwa ndoto yake ni kuendesha watalii, tatizo kubwa barabarani ni ujuaji na ubabe wa baadhi ya madereva wanapokuwa barabarani Hali inayopelekea ajali nyingi kutokea.
“Hapa naona msisitizo wa nidhamu barabarani kwani madereva wengi wanazijua sheria, kanuni na taratibu lakini kiburi au kuona sifa katika uvunjaji wa sheria ni kama ufahari kwao, ikiwemo mwendo kasi, kuyapita magari mengine au hata kutokufuata alama za barabarani na taa zake”amesema.
Aidha ameiomba Serikali kuunda kifurushi cha kupumzisha baadhi ya madereva watakaobainika kusababisha ajali kwa uzembe wafutiwe lesseni kwa miezi sita au mwaka kulingana na ukubwa wa kosa.