Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, akizungumza na waandishi wa habari wakati alipoziagiza taasisi zinazodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kulipa madeni haraka kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilipotembelea MSD.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai akifafanua mambo mbalimbali mara baada ya kumalizika kwa ziara ya Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilipotembelea MSD.
………………………………………..
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, ameziagiza taasisi zinazodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) kulipa madeni haraka kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Ameyasema hayo Septemba 13,2023 wakati Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilipotembelea MSD na kuelezwa kuwa inadai zaidi ya Sh bilioni 20 kutoka katika taasisi mbalimbali za umma.
“Mteja akishatoa huduma anatakiwa alipwe haraka na hayo ndiyo maelekezo ya mheshimiwa Rais kwamba ndani ya siku 60 mtoa huduma awe amelipwa, lakini bima wanachelewesha fedha, hilo tutalisimamia kwa karibu na tutawaelekeza walifanyie kazi haraka,” amesema Dk. Mollel.
Kuhusu ushuru unaotozwa MSD kwa dawa na vifaa tiba vinavyosafirishwa kwenda Mafia amesema watawasiliana na wizara husika kutatua changamoto hiyo.
Dk. Mollel pia ameziagiza halmashauri kukadiria dawa kulingana na mahitaji yaliyopo kwenye maeneo yao kuepuka kukosekana kwa dawa katika vituo vya afya.
“Najua kuna magonjwa yanayotokea ambayo hayajapangwa, tuna namna ya kushughulika nayo lakini yale yaliyozoeleka wakadirie kwa thamani halisi,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, amesema wanaendelea na utekelezaji wa mikakati mbalimbali waliyoiweka sambamba na ujenzi wa maghala mawili ambapo tayari la Mtwara limeanza.
Meneja wa MSD Kanda ya Mashariki, Betia Kaema, amesema wanahudumia vituo 966 kwenye halmashauri 23 za Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Zanzibar inadai zaidi ya Sh bilioni 20 kutoka katika taasisi mbalimbali za umma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Stanslaus Nyongo, ameitaka NHIF kulipa madeni kwa wakati ili hospitali zinazodaiwa ziweze kulipa madeni MSD.
“Tutaongea na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya waweze kulipa madeni ili MSD iendelee na kazi zake za kupelea dawa kwa wakati.” Amesema Nyongo.