Wajasiriamali 22 wanaojihusisha na utengenezaji mkaa mbadala wamepatiwa mafunzo na Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Umaskini (REPOA) ili waweze kufahamu njia bora za uzalishaji wa nishati hiyo.
Akizungumza Septemba 12,2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uzalishaji mkaa mbadala kwa wajasiriamali hao, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa nchi wenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
Amesema mafunzo hayo yametayarishwa baada ya kufanyika utafiti katika mikoa 12 hapa nchini na kutembelea wazalishaji mkaa mbadala 58 na watumiaji 122.
“Utafiti ulifanywa na TIRDO kwa kushirikiana na REPOA ukiwa na lengo la kuimarisha uzalishaji wa mkaa mbadala na kukuza matumizi yake kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini,” amesema Profesa Mtambo.
Aidha amesema watafiti walichukua sampuli 43 za mkaa mbadala kutoka kwa wazalishaji katika mikoa hiyo na kupima kwenye maabara ambapo matokeo ndiyo yaliyopelekea mashirika hayo kufanya uboreshaji baada ya kubaini changamoto za viwango na ubora unaotakiwa.
Amesema pia watafiti wamesanifu mashine ya kuchomea malighafi za bayomasi yenye uwezo wa kupunguza niashati ya kuchomea kwa asilimia 50, kuvuna joto ambalo linatumika kukaushia mkaa na kuvuna vinega.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa REPOA, Dk. Donald Mmari, amesema wazalishaji wengi bado hawana ujuzi wa kutosha kuzalisha mkaa mbadala wenye viwango vinavyokubalika katika matumizi.
Amesema mkaa mbadala utasaidia kutunza mazingira na misitu kwa sababu asilimia 85 ya Watanzania wanatumia mkaa unaotokana na miti.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazalishaji na Wasambazaji wa Nishati Safi Tanzania, Phinias Magesa, ameishukuru Serikali kwa kuanza kuwatambua wazalishaji wa mkaa mbadala na kusema hatua hiyo itasaidia kupunguza ukataji miti.