Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni amewataka wafugaji wa asili ya wilayani hiyo kuhakikisha wanafuga kisasa na kuacha kufuga kimazoea ili kuepuka athari zinazotokana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo mifugo mingi hufa kwa kukosa malisho.
Kasilda ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa soko jipya la mnada wa ng’ombe na mazao mbalimbali ya chakula lengo ni kukuza uchumi wa wilaya hiyo na wafugaji hao kuuza mifugo kabla ya Kipindi cha ukame kuanza ni muda muafaka sasa wafugaji hao kutumia soko jipya la mnada Kirinjiko lililopo wilayani humo Kwa kuuzia mifugo yao.
DC Kasilda aliendelea kusema Serikali imewawekea mazingira mazuri ikiwemo miundo mbinu ya kisasa Kwa ajili ya Kuendesha mnada Katika eneo hilo.
Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwakuelekeza fedha nyingi kwenye miradi ya Maendeleo ikiwemo kwenye Sekta ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi, Afya, Elimu pamoja na miundombinu ya Barabara na Maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo Anastasia Tutuba amesema mpaka Sasa kwenye eneo hilo Halmashauri imeshapima vizimba zaidi ya 600 na kwamba kama Halmashauri wataendelea kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana katika eneo hilo lengo likiwa ni kuiongezea Halmashauri mapato na kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya hiyo.