Na Victor Masangu,Pwani
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani katika kupambana na kudhibiti mianya ya ulipaji wa kodi imezindua kampeni maalumu yenye lengo la kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu kutumia mashine za kielekroniki (EFD) pindi wanapouza bidhaa zao.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Masawa Masatu wakati akizungumza na waandishi kuhusiana na kampeni hiyo ambayo pia itaenda sambamba na kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanasai risiti pindi wanapofanya manunuzi kwani ni haki yao ya msingi.
Meneja Masawa alisema kwamba kampeni hiyo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara waweze kutimiza wajibu wao katika suala zima la ulipaji wa kodi kwa hiari bila ya kukwepa lengo ikiwa ni kuisaidia serikali kukusanya mapato yake.
“Kikubwa nimewaita kwa ajili ya kampeni hii maalumu ambayo itajulikana kwa jina la Tuwajibike,’kodi yetu maendeleo yetu’ na kikubwa ni kutoa elimu katika Wilaya mbali mbali za Mkoa wa Pwani na kikubwa ni wafanyabiashara kulipa kodi ili kuisaidia serikali,”alisema Masawa.
Alifafanua kuwa wananchi wanapaswa kuhakikisha wanasai risiti zao halali pindi wanaponunua bidhaa zao na pia wafanyabiashara watoe risiti za kielectoniki pindi wanapouza bidhaa zao kwani kufanya hivyo kunasaidia serikali kupata mapato yake kihalali.
Aidha Meneja huyo alibainisha kuwa lengo kubwa ni kuweka mikakati madhubuti katika ukusanyaji wa kodi ambayo itaweza kusaidia katika mambo mbali mbali ikiwemo kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile ya elimu,afya,umeme,pamoja maeneo mengine.
Nao baadhi ya wafanyabiashara wa Mkoani Pwani hawakusita kuzungumzia juu ya umuhimu wa kutumia mashine hizo za EFD huku wameipongeza TRA kwa hatua ya kwenda kuwatembea na kuwapa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maslahi ya maendeleo ya Taifa.
Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo la Loliondo alibainisha kuwa kutokana na elimu ambayo wamekuwa wakiipata kutoka kaa TRA Mkoa wa Pwani kumewasaidia wateja wao kusai risiti zao baada ya kumaliza kufanya manunuzi ya bidhaa zao.
Kampeni hiyo maalumu ambayo imepewa jina la Tuwajibike itafanyika kwa kipindi cha wiki moja katika Wilaya mbalu mbali za Mkoa wa Pwani ambapo italenha zaidi kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara juu ya kutoa risiti halali pamoja na kudai risiti.