Mkuu wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro,Kasilda Mgeni ametoa onyo kali kwa Mwekezaji wa kampuni ya uwekezaji ya LM Investment inayozalisha Katani Wilayani hapo ambayo hivi karibuni imezua mjadala mkali mitandaoni uliosababisha taharuki kwa kuwashutumu wanakijiji wa kata ya Maore Wilayani hapo kuvamia eneo lake la uwekezaji kwa kukata na kuchoma mikonge yake.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo wakati akizungumza na wanavijiji vitatu vya Mpirani,Msufini na Ndungu Jana Septemba 10 ambapo amemtaka mwekezaji huyo kuacha mara moja kusambaza mitandaoni taarifa za uongo zenye kuzua taharuki na zenye kuichonganisha serikali na Wananchi jambo linaloharibu taswira ya serikali ionekane kwamba haiwajali wawekezaji,kitu ambacho si cha kweli,bali kazi ya Serikali ni kuondoa kero,kulinda wawekezaji na kutetea wanyonge.
“Mimi nitumie Mkutano huu kumuonya mwekezaji juu ya vitendo vyake vya taharuki ya kudanganya watanzania kwamba Wananchi wa Ndungu,Msufini na Mpirani wanavamia maeneo yake na kuchoma mkonge,Nampa onyo atakaporudia tena serikali haitamwacha tutamchukulia hatua za kisheria kwasababu anaichonganisha serikali na wananchi” amesema Mgeni
Mgeni ameongeza kwa kuwataka wanakijiji wa kata ya Maore wawe na mahusiano mazuri na mwekezaji ili kuwepo na Maendeleo yenye tija kati ya mwekezaji na wanakijiiji huku akiwataka kuhakisha zoezi la malipo ya ankara ya umilikishwaji wa viwanja hekta 300 walizopewa na serikali ya Tanzania yanafanyika mapema.
Aidha mkuu wa wilaya huyo ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Same kukamilisha ndani ya wiki moja zoezi la uwekaji wa alama za mipaka mikubwa itakayotenganisha eneo la mwekezaji na la Kijiji ili mwekezaji asipate sababu nyingine ya kuzusha taarifa za uongo kama alizozizusha hapo awali.
Wakati huohuo Diwani wa kata ya Maore,Abedi Ally amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuwapa matumaini wanakijiji hao kwamba ardhi hiyo ni Mali yao si ya mwekezaji tena huku akiwasisitiza wanakijiiji ambao bado hawajalipia viwanja vyao wavilipie mapema ili zoezi la kukabidhi maeneo hayo lifanyike mapema wiki ijayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kata ya Maore,Rajabu Kijangwa na Yasin Hassan wamesema wanamshukuru mkuu wa wilaya kuliingilia kati jambo hilo ambalo limekuwa likiwanyima furaha kutokana na tabia ya mwekezaji huo ambaye amekuwa akisafisha shamba lake kwa kuchoma nyasi Kisha kurekodi video na kuisambaza mtandaoni huku akidai kuwa ni wanakijiji wa Maore ndio wamefanya hivyo kwamba wamevamia eneo lake kwa kulichoma moto kitu ambacho si kweli.
Hata hivyo mwekezaji huyo,Omari Mndeme amesema kuwa wanakijiji wa kata hiyo wamemdanganya mkuu wa wilaya kuwa hakuna eneo lililochomwa wala kukatwa mikonge ilihali zipotakribani hekari mbili ambazo zimechomwa na kukatwa mikonge na wanakijiji hao ambapo amesema kunawakati mwingine amekuwa akitishiwa na mapanga na hatua alizochukua ni kwamba ameshatuma barua kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wizara ya ardhi ambapo anategemea kujibiwa hivi karibuni.
Ikumbukwe hivi karibuni Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi , Mhe. Georfrey Pinda alikwenda kwenye vijiji hivyo vitatu vya Msufini,Mpirani na Ndungu ambapo aliwakabidhi rasmi hekari 300 kwa wananchi ambapo kila kijiji kiligawiwa hekari mia moja na kwamba alimtaka mwekezaji huyo kutowabughudhi wananchi hao kwani ardhi hiyo wamepewa na Rais ni rasmi imeidhinishwa kuwa ni mali yao .