Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu anatarajiwa kuanza ziara ya siku tatu kuanzia Septemba 11-13, 2023 katika Mkoa wa Songwe kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe, Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati.
Kwa mujibu wa taarifa, iliyotolewa kwenye kurasa za mtandaoni za Wizara ya Afya leo Septemba 10, 2023 zimebainisha kuwa Waziri Ummy pia atazungumza na Timu za usimamizi Huduma za Afya ya Mkoa (RHMT) na za Halmashauri (CHMT’s) na kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa Septemba 11, 2023 Waziri Ummy anatarajiwa atakuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Septemba 12, 2023 katika Wilaya ya Momba na atamalizia Ziara hiyo Septemba 13,2023 katika Wilaya ya Mbozi.