Kongamano la Kimataifa la Sita la Magonjwa ya Ini Barani Afrika (COLDA) limezinduliwa jijini Dar es Salaam ambapo limekutanisha wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa chakula na Ini, kutoka katika nchi 43 kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kukabiliana na kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula na Ini.
Akizindua kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Pascal Ruggajo amesema kuwa ni heshima kubwa kama nchi kuwa mwenyeji wa kongamano hilo kubwa ambalo limekutanisha wataalamu wa kada mbalimbali ikiwemo Wataalamu wa Uchunguzi, Radiolojia, Wapasuaji, Wataalamu wa Mionzi na dawa.
Prof. Ruggajo amesema Magonjwa ya ini barani Afrika na duniani kwa ujumla yanaongezeka kwa kasi, ambapo Tanzania inakadiriwa kuwa kati ya watu 100 basi watu 4 Hadi 8 wana maambukizi ya homa ya Ini.
Prof. Ruggajo amesema Wizara ya afya inaandaa sera ya kukabili magonjwa mbalimbali inayojumisha Magonjwa ya VVU, Magonjwa ya ngono na Hepatitis B.
“Serikali imejipanga kukabiliana na magonjwa ya ini kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa vya uchunguzi na tayari wataalamu kadhaa wa magonjwa ya homa ya ini wamepatiwa mafunzo nje ya nchi”. Ameeleza Prof. Ruggajo.
Aidha, Prof. Ruggajo ametoa wito kwa wananchi kufanya uchunguzi wa magonjwa ya Ini na kupata chanjo.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa Hospitali hiyo ni kituo kimojawapo cha kushughulikia matatizo ya ini na Mfumo wa Chakula kati ya vituo vinne vilivyopo afrika, ambapo vituo vingine vipo Morocco, Misri na Afrika kusini na kwamba tayari kituo hicho kina wataalamu wenye weledi wa kutibu changamoto mbalimbali za magonjwa hayo.
Kongamano la COLDA linafanyika nchini kwa siku tatu ambapo awali lilitanguliwa na mafunzo ya kutibu magonjwa ya ini na mfumo wa chakula kwa kutumia matundu madogo.