Na Sophia Kingimali
Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amebainisha kuwa mbolea nyingi inayotumika Afrika inatoka nje ya bara hilo, wakati ile inayotengenezwa Afrika inauzwa nje ya bara hilo.
Hayo yamebainishwa Septemba 6 wakati akizungumza kando ya mkutano wa Mifumo ya Chakula Barani Afrika(AGRF )wakati wa majadiliano kuhusu ajenda ya mbolea Barani Afrika na afya ya udongo iliyofanyika katika ukumbi wa Selous ndani ya jengo la mikutano ya kimataifa la Julius K. Nyerere Jijini Dar Es Salaam.
Waziri Mkuu mstaafu Pinda amesema, zaidi ya asilimia 90 ya mbolea nchini inaagizwa kutoka nje huku chini ya asilimia kumi ikitengenezwa ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa, kwa sasa mbolea inayopatikana nchini inatoka nchi mbalimbali ikiwemo Russia, na kwa sasa upatikanaji wake umekuwa na changamoto kutokana na vita inayoendelea katika nchi hiyo.
Pinda ameongeza kuwa, hali hiyo imesababisha bei ya mbolea kupanda na pia mbolea kuadimika na kufikia kuhatarisha usalama wa chakula kwa baadhi ya nchi za Afrika.
Ameongeza kuwa, kutokana na bei ya mbolea kupanda duniani, Serikali za nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania zimeanzisha programu wezeshi za kusaidia upatikanaji wa mbolea ili kuleta suluhu ya changamoto hiyo kwa kuweka ruzuku kwenye pembejeo hiyo.
Kwa upande mwingine Pinda amesema matumizi ya mbolea yasiyofaa yamechangia kuzorotesha afya ya udongo na kusababisha mavuno kuwa hafifu.
Akizungumza alipokuwa akikaribisha mjadala kuhusu tasnia ya mbolea na afya ya udongo Rais wa Agra Afrika Dr. Agness Kalebata amesema asilimia hamsini (50%) ya chakula kinacholiwa duniani kinazalishwa kwa kutumia mbolea.
Ameongeza kuwa, matumizi ya mbolea yameendelea kuwa hafifu kutokana na upatikanaji wake kuwa mdogo na hivyo kupelekea uzalishaji mdogo wa mazao.
Kwa upande wake mmoja wa Pannelist ameeeleza kuwa, bara la Afrika linahitaji kuongeza uzalishaji wa mbolea ili kupunguza utegemezi kutoka nchi zilizoendelea na hivyo kutuhakikishia afya bora ya udongo unaotumika katika kuzalisha mazao.
Ameongeza kuwa, udongo unahitaji virutubisho kama vile mwili wa mwanadamu unavyohitaji ili uendelee kuzalisha na kuleta tija kwa wakulima.
Imeshauriwa serikali mbalimbali barani Afrika kufanya kazi bega kwa bega na taasisi binafsi ili kutatua changamoto ya pembejeo ya mbolea.
Kufanya kazi, kuboresha mbegu na kuhakikisha mbolea bora inapatikana kwa wakati sahihi na mahala sahihi kutawawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kuinua vipato vyao.