Na Dennis Gondwe, CHANG’OMBE
WANANCHI wa Kata ya Chang’ombe wametakiwa kujitokeza na kukitumia Kituo cha Afya Chang’ombe ambacho kimeanza kutoa huduma za kiwango cha juu.
Kauli hiyo ilitokewa na Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikila apokuwa akiongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa uliofanyika katika Mtaa wa Chilewa katika Kata ya Chang’ombe Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Diwani Fundikila alisema kuwa Kituo cha Afya Chang’ombe kimeanza kutoa huduma bora.
“Ndugu zangu niwatangazie rasmi muende mkapate huduma kituoni pale. Serikali metatua changamoto ya kituo cha afya, sasa msihangaike kwenda maeneo ya mbali. Tumewajengea kituo cha afya kata ya Chang’ombe nendeni mkapate huduma pale.
Kituo kile tulipewa shilingi 500,000,000 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kukijenga kituo chetu na kazi bado inaendelea ya ujenzi wa kituo chetu kiweze kukamilika. Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu, tuendelee kumuunga mkono mbunge wetu wa Dodoma mjini, na tuendelee kuwaunga mkono viongozi wa serikali za mikaa na chama chetu” alisema Fundikila.
Wakati huohuo, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwa Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde na kumteua kuwa waziri wa Madini.
“Tunae Mheshimiwa Anthony Mavunde, hivi karibuni Mheshimiwa Rais amempa cheo kikubwa sana cha Waziri wa Madini na ameshaapa. Tunampongeza sana lakini pongezi zaidi anastahili Mheshimiwa Rais kwa kuona anafaa” alisema Fundikila.
Chama cha Mapinduzi Kata ya Chang’ombe kinafanya ziara ya kikazi katika Matawi yote ya chama hicho kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kuwashukuru wanachama wake kwa kuchagua uongozi wa CCM Kata ya Chang’ombe.