NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza limezindua sherehe na maonyesho ya Maulidi ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.W.A. na kuwataka waumini wa dini zote kuhudhuria.
Pia limewataka Watanzania kwa umoja wao kujitokeza kupira kura kwenye uchaguzi a serikali za mitaa mwaka huu ili kuchagua viongozi waadilifu weny hofu ya Mungu kwa sababu uimara wa serikali unaanzia chini.
Kaimu Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hassani Kabeke alisema jijini humu wakati akizindua sherehe za Maulidi ya kuzaliwa Mtume Muhammad S.W.A zinazofanyika kitaifa mkoani humu.
Alisema wananchi na wakazi wa Jiji la Mwanza waislamu na wasio waislamu wajitokeze kwenye maulidi hayo ya kuzaliwa kwa Mtume na waonyeshe ukarimu wao kwa wageni wa ndani na nje ya nchi watakaohudhuria sherehe hizo ambazo mgeni rasmi atakuwa Mufti Abubakar Zuberi.
Sheikhe Kabeke alieleza kuwa Novemba 9, kabla kutafanyika matembezi ya amani (Zafa) yatakayoongozwa na Ngamia wawili na kupokewa na Mutfi, yakianzia BAKWATA mkoa kupitia barabara ya Nyerere hadi Viwanja vya Furahisha, Manispaa ya Ilemela ambapo kabla maandamano hayo kutakuwa na siku maalumu ya kuombea nchi idumu katika amani na utulivu.
“Tumezindua rasmi leo maonyesho na sherehe za maulidi ya Mtume Muhammad S.A.W ambayo ni siku yake ya kuzaliwa na kilele chake kitakuwa Novemba 9, mwaka huu, kutakuwa na maonyesho ya shughuli za kijamii,upimaji wa kisukari,macho, shinikizo la damu na uchangiaji wa damu wa hiari unaolenga kukusanya chupa 8,000 ili kuokoa maisha ya watu kama alivyofanya Mtume,”alisema Sheikhe Kabeke.
Sheikhe huyo wa mkoa aliwahamasisha wananchi wa jiji hili kufanya usafi kwenye mitaa yao, makazi, barabara na kupaka rangi nyumba huku akiwashauri waumini wa dini ya Kiislamu kuunda vikundi vya kupita nyumba kwa nyumba ili kuwaalika waumini wa dini zingine washiriki maulidi.
Aidha, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, aliwataka wanasiasa wasiharibu nchi kwa uchu wa madaraka, bali wafahamu kuna watanzania zaidi ya watu milioni 55 ilhali vyama vyao vikiwa na wananchama wasiozi milioni 30.
Pia aliwahamiza watanzania hasa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi waadilifu na wenye hofu ya Mungu kwani uimara wa serikali unaanzia chini na itakuwa busara wanasiasa wakaongeza juhudi ili uchaguzi ufanyike kwa amani,usalama na utulivu badala ya kusababisha migogoro inayoweza kuharibu nchi.