Upasuaji ukiendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Dakitari bingwa wa upasuaji sanifu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Francis Tegete (katikati)akiwa na madakitari wabobezi kutoka Chuo kikuu cha Duke Marekani wakizungumza na waandishi wa habari.
Upasuaji ukiendelea kwenye chumba cha upasuaji katika Hospital ya Bugando
……..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Madaktari wabobezi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC) kwakushirikiana na madakitari kutoka Chuo kikuu cha Duke kilichopo Marekani wamefanya upasuaji wa kurekebisha sura kwa wagonjwa 35.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Agosti 25, 2023 Daktari Bingwa wa upasuaji sanifu kutoka Hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando Francis Tegete, amesema wamekuwa na kambi ya madaktari hao kutoka Marekani kwa lengo la kufanya upasuaji bobezi wa kurekebisha sura za wagonjwa zilizoharibika kutokana na ajali mbalimbali ikiwemo ya moto ambapo upasuaji huo umefanyika kwa muda wa siku tano.
Amesema kambi ya upasuaji sanifu imeshirikiana vizuri na idara ya mabingwa wa upasuaji wa pua,koo na masikio ili kuweza kufikia malengo ya Hospitali ya kuelekea kwenye upasuaji bobezi huku akiongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya afya imeamua kuwekeza juhudi kwa wataalamu wake wa ndani kwakuwaunganisha na wataalamu mbalimbali wa afya Duniani ili wazidi kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa.
” Wagonjwa ambao wanakuwa na shida kwenye maeneo ya shingo, kichwani na usoni mara nyingi ni matatizo ambayo yanawafanya jamii iwanyanyapae na kushindwa kuchangamana nao, matibabu hayo ni makubwa yanahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo kuwa na timu hii kutoka Marekani inatusadia sisi kujijengea uwezo hatua itakayosaidia huduma hii kuenea kwa haraka hapa nchini”,amesema Dkt.Tegete
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na mbobezi wa upasuaji wa kiuno na nyonga Stephene Swetala, amesema Udaktari wa fundi sanifu ni moja ya upasuaji ambao ni adimu sana na kwa Kanda ya ziwa ni Hospitali ya Bugando ndio wanatoa huduma hiyo na Tanzania kuna madaktari wachache kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Manoj Abraham ni miongoni mwa madaktari bingwa kutoka chuo cha Duke Marekani amesema wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na madaktari wa Bugando huku akiwasihi kuipeleka huduma hiyo mbali zaidi ikiwemo kuwafundisha vizazi vijavyo.
Grace Rwechungula ni miongoni mwa waliofanyiwa upasuaji amewashukuru Madaktari hao kwakumpa huduma nzuri