Na. Sixmund Begashe
Ugunduzi wa maeneo mapya ya masalia ya binadamu wa kale, zana za Mawe na michoro ya Miambani Siuyu Wilaya ya Ikungi, unakwenda kuufungua zaidi Mkoa wa Singida kiutalii wa Akiolojia, Utamaduni na Malikale.
Akizungumza na watafiti wa Akiolojia wa ndani na nje ya nchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Bw. Rashid Mohd Rashid ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale nchini, kwa juhudi inazozichukua katika tafiti zinazoibua maeneo mapya yenye historia adhimu ya Binadamu wa kale na shughuli zao hususani eneo la Siuyu Mkoani Singida.
Bw. Rashid akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Bw. Justus Kijazi, ametoa wito kwa jamii kuhakikisha maeneo hayo ya Malikale yanalindwa kwa maslahi mapana ya wanaikungi na Taifa kwa ujumla, huku akiahidi kuwa Serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili katika uhifadhi na kutangaza vivutio vya Malikale kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu amesema matokeo chanya ya tatifi zinazofanywa licha tu ya kuongeza kasi ya utalii na uchumi wa nchi pia zinatoa elimu kwa jamii juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi na umuhimu wa uhifadhi endelevu na utunzaji wa mazingira.
Dkt. Ntandu ameongeza kuwa Idara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na taasisi pamoja na wadau mbalimbali katika kuelimisha umma juu ya umuhimu wa uhifadhi wa maeneo ya kihistoria.
Naye Mtafiti wa akiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Sapienza nchini Italia, Prof. Marina Gallinaro ameeleza kuwa kutokana na utajiri mkubwa wa maeneo ya Malikale hapa nchini hasa Mkoani Singida, amevutiwa kuja nchini kuungana na watafiti wa nchini Tanzania kufanya utafiti.
Akielezea tafiti zinazofanyika Ikungi kwa kushirikiana na Watafiti kutoka nchini, Italia, Ethiopia na Ufarasa, Mtafiti wa Akiolojia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dkt. Makarius Peter Itambu, amesema hadi sasa wamefanikiwa kugundua fuvu la binadamu wa kale anaesadikika kuishi zaidi ya miaka mia 7 iliyopita na zana za mawe za pili na za mwisho.
Tafiti hizi pia katika Mkoa wa Singida zimegundua Michoro ya kwenye miamba, na zana za mawe za muhula wa kwanza na wa pili zilizotumika zaidi ya miaka laki 3 iliyopita.