Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano katika shule ya msingi Mgombe iliyopo katika halmasahuri ya Mlele mkoani Katavi yamekuwa kivutio kikubwa kwa wazazi wanaoishi maeneo hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya awli iliyotolewa kwa Kiongozi wa Mbio za Uhuru Kiaifa, Abdallah Shaib Kaim, mradi huo wa vyumba viwili vya madarasa ya awali ya mfano katika shule ya msingi mgombe ni utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014; inayoelekeza mamlaka ya serikali za mitaa kuhusika katika uanzishaji, usimamizi na uendeshaji wa shule za elimu ya awali.
Halmashauri ya mlele kwa kushirikiana na serikali katika imetekeleza mradi huo baada ya kupokea kiasi cha shilingi 55,824,000 za mpango wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa elimu ya msingi awamu ya pili chini ya ufadhili wa Global Partnership for Education (GPE LANES II)
Mradi huo unahusissha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, matundu 6 ya vyoo, meza za watoto 30 na viti vya watoto 30.
Vingine ni pamoja na viti viwili vya walimu, vizimia moto, mikeka ya kukalia watoto kumi na bembea.
Utekelezaji wa mradi ulianza Septemba mosi mwaka 2022 na kukamilika tarehe 30 Disemba 2022 ambapo madarasa hayo yalianza kutumika na wanafunzi wa awali tarehe 9 Januari 2023.
Mara baada ya kukagua mradi huo Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa alisema ameridhishwa na ubora wake.
‘Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 zimeridhika na utekelezaji wa mradi huu ambao umeboresha mazingira ya ufundishwaji kwa watoto wa darasa la awali, na hapana shaka ninakwenda kuuzindua rasmi mradi huo’ alisema Kaim.
Mradi huo pia unaelezwa kupunguza msongamano wa wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo, ambapo walikuwa wakitumia chumba kimoja kwa wastani wa wanafunzi 70 lakini sasa wastani wa wanafunzi kwa chumba kimoja ni 35.
Wakizungumzia mabadiliko hayo baadhi ya wazazi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi akiwemo Maria Paskali na Joselina Mafuru walisema madarasa hayo yanahamasisha wazazi kuandikisha watoto shule mapema.
‘Ukilinganisha na madarasa hayo ya zamani kwa kweli haya ni mazuri mno hata ukileta mtoto humo una uhakika wa mtoto kurudi nyumbani msafi’ alisema Joselina.
‘Hata ukitizama tu hivi haya madarasa ni mazuri kwakweli unatamani urudi utoto ili usomee mahali pazuri hivi’ alisema Maria.