Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Justin Nyamoga wakiwa katika ziara ya kukagua mradi wa awamu ya tatu wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) ambao unatoka katikati ya mji hadi Gongo la Mboto leo Agosti 27,2023 Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Edwin Mhede (wa pili kutoka kulia) akitoa ufafanuzi kwa Makamu Mwenyekiti Kamati ya kudumu ya bunge ya TAMISEMI Mhe. Justin Nyamoga (wa kwanza kushoto) wakati Kamati ya Kuduma ya Bunge ya TAMISEMI wakikagua mradi wa awamu ya tatu wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kutoka katikati ya mji hadi Gongo la Mboto.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na ujenzi wa mradi wa awamu ya tatu wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kutoka katikati ya mji hadi Gongo la Mboto.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Edwin Mhede akifafanua jambo kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kamati ya kudumu ya bunge ya TAMISEMI imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Dar es Salaam awamu ya tatu, huku wakitoa wito kwa mamlaka husika kuongeza idadi ya mabasi ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma bora na kufikia malengo tarajiwa.
Akizungumza leo Agosti 27, 2023 jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti Kamati ya kudumu ya bunge ya TAMISEMI Mhe. Justin Nyamoga, amesema kuwa wakati umefika wa BRT kuanza kutumia teknolojia kwa kutumia smart card jambo ambalo ni rafiki kwa abiria katika kutatua changamoto.
Mhe. Nyamonga amesema kuwa mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa mapato ni muhimu ili kuleta tija katika utendaji pamoja na kufikia malengo husika.
“Tunawapongeza kwa kutumia wataalamu wa ndani pamoja na kuhakikisha mnaendelea kulinda mifumo, uendelee kuwa wazalendo katika utendaji kazi” amesema Mhe. Nyamonga.
Hata hivyo amesema kuwa serikali inapaswa kutenga maeneo katika miji inayokuwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ili kuepuka kulipa watu fidia wakati wa uendelezaji miradi mbalimbali.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dkt. Edwin Mhede, amesema kuwa kamati ya kudumu ya bunge ya TAMISEMI wametembelea mradi wa awamu ya tatu wa BRT ambao unatoka katikati ya mji kwenda Gongo la Mboto.
Dkt. Mhede amesema kuwa mpaka sasa utekelezaji ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa usafiri haraka wa mabasi (BRT) umefikia asilimia 17.65.
Amebainisha kuwa mradi unatarajiwa kukamilika marchi 2024 huku akieleza kuwa mafundi wanaendelea na ujenzi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
“Pia wabunge wamaona changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa maradi huu ikiwemo vumbi ambalo linakwenda katika makazi ya watu wakati wa uekelezaji wa mradi huu, na tayari wataalamu wameanza kudhibiti ili kuepuka madhara” amesema Dkt. Mhede.
Dkt. Mhede amesema kuwa wanaendelea kujipanga ili kasi ya ujenzi wa miundombinu iendane na idadi ya mabasi yaendayo jambo ambalo litasaidia kuleta tija na kufikia malengo tarajiwa.