Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi Ofisi ya Makamu wa Rais, Juliana Mkalimoto akizungumza na Maafisa Ununuzi na Ugavi wakati wa kufunga warsha ya mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni iliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Jumapili Agosti 27, 2023.
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira wa ofisi hiyo, Dkt. Deogratius Paul akitoa hotuba ya kufunga mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni iliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Jumapili Agosti 27, 2023.
Baadhi ya Maafisa ununuzi na ugavi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Umma wakifuatilia hotuba ya kufunga mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni iliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Jumapili Agosti 27, 2023.
Baadhi ya Maafisa ununuzi na ugavi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Umma wakifuatilia hotuba ya kufunga kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni iliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar Jijini Dodoma leo Jumapili Agosti 27, 2023.
Mhandisi Goodluck Rulagora kutoka Chuo cha Uvuvi Bagamoyo (FETA) akitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi vya kemikali vinavyotumika katika vifaa mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi kwa maaafisa ununuzi na ugavi wakati wa mafunzo kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni leo Jumapili Agosti 27, 2023 Jijini Dodoma.
…………………………
Na Mwandishi Wetu,
DODOMA
27.8.2023
WATAALAMU wa ununuzi na ugavi Serikalini wamehimizwa kuzingatia miongozo ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuepuka manunuzi vifaa vyenye ukomo wa matumizi ambavyo husababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu na mazingira.
Hayo yamesemwa leo Jumapili (Agosti 27, 2023) Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi wa Ofisi hiyo, Juliana Mkalimoto wakati akifunga warsha ya siku mbili ya mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi kuhusu utekelezaji wa itifaki ya montreal inayohusu kemikali zinazomongonyoa tabaka la ozoni.
Mkalimoto amesema maafisa ununuzi na ugavi ni wadau muhimu wanaopaswa kuzingatia utekelezaji wa itifaki ya Montreal kwa kuwa ndio wahusika wakuu wa huduma ya manunuzi wa vifaa na vitendea kazi mbalimbali vinavyotumika na Serikali kupitia Wizara, Idara na Taasisi za umma katika kutekeleza majukumu yake kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mkalimoto amesema Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya huduma za ununuzi na ugavi katika utoaji wa huduma, hivyo ni wajibu wa Maafisa ununuzi na ugavi kuzingatia thamani ya fedha wakati wa kushindanisha zabuni mbalimbali.
Kama mnavyofahamu Serikali inaendelea na ujenzi wa majengo katika maeneo mbalimbali nchini na mfano mzuri ni kule Mtumba (Dodoma)Tukiwa kama wataalamu tunapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa michakato ya zabuni ili kuepuka uagizaji na uingizaji wa vifaa vyenye ukomo wa matumizi ambavyo vina madhara ya afya kwa binadamu na mazingira amesema Mkalimoto.
Aidha Mkalimoto amesema kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo kwa watumishi wa kada ya ununuzi na ugavi, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudia kutoa mafunzo hayo kwa maafisa ununuzi na ugavi waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekretarieri za Mikoa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema mafunzo hayo ni moja ya juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa elimu kuhusu udhibiti wa vifaa vya kemikali inaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali katika jamii.
Tumepanga mafunzo haya pia yatolewe kwa upande wa Zanzibar kwa kuwa kule kuna bandari ambayo inatumika kuingiza na kupokea bidhaa za aina mbalimbali ikiwemo kemikali.Tumekusudia mafunzo haya kuwa endelevu ili tuweze kujenga uelewa wa pamoja kwa jamii amesema Kemilembe.
Naye Afisa Ununuzi na Ugavi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Stanslaus Kagali ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mafunzo hayo yamewapa uelewa kuhusu umuhimu wa ukomo wa matumizi ya vifaa vyenye kemikali ikiwemo majokofu na ambavyo mara kwa mara vimekuwa vikinunuliwa na Serikali.
“Asilimia 75 ya fedha za Serikali zinahusiana na huduma za ununuzi na ugavi…Tunashukuru kupatiwa mafunzo haya kwa kuwa yanatuwezesha kubaini aina ya vifaa ambavyo havifai kwa ajili ya matumizi kutokana na madhara yake kwa afya ya binadamu na mazingira amesema Kagali.
Mafunzo hayo ya siku mbili yashirikisha jumla ya maafisa ununuzi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na Watoa mada kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).