………………….
Na Sixmund J. Begashe
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale nchini imeendelea na jitihada zake za kuhakikisha maeneo ya Urithi wa Kihistoria hususani yaliyopo Kilimatinde, Manyoni Mkoa wa Singida, ambayo hayatambuliki yanatambuliwa, kuhifadhiwa kisheria na Kutangazwa ili yachochee kasi ya Utalii nchini.
Akizungumza na Uongozi wa Serikali ya Kata ya Kilimatinde pamoja na Wazee wa eneo hilo, Mkurugenzi wa Malikale Dkt. Christowaja Ntandu, ameeleza kuwa, Kilimatinde inautajiri Mkubwa wa Urithi wa Malikale hivyo ni dhamira ya Wizara kuhakikisha maeneo yote yanaainishwa, ili yahifadhiwe kisheria, Kutangazwa ili watalii wamiminike katika eneo hilo.
Dkt. Ntandu ameupongeza uongozi wa Serikali ya Kilimatinde na wanachi kwa ujumla kwa kuhifadhi Urithi wa kihistoria uliopo eneo hilo na kuwahakikishia kuwa Wizara kupitia Idara anayoiongoza kwa kushirikiana na Wananchi wa eneo husika kuendelea kuhifadhi na kulitangaza ili kukuza Utalii zaidi wa Kihistoria katika eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kilimatinde, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua inazozichukua za Kuainisha maeneo mapya ya Malikale kwenye eneo la Kilimatinde kwani yanakwenda kuinua uchumi wa Wananchi wa Kilimatinde na Taifa kwa ujumla huku akiwataka wananchi kuendelea kuyalinda.
Kilimatinde ni moja ya maeneo machache nchini yaliyo pitiwa na Njia ya kati ya Biashara Utumwa na Meno ya Tembo, pia ilikuwa ni ngome ya kwanza iliyowekwa na ukoloni wa Kijerumani na kuanza kutumika Mwaka 1891, na baadae kukaliwa na Ukoloni wa Uingereza 1922.
Aidha eneo hilo pia lina majengo ya kwanza yaliyotumika kutolea huduma za kijamii na elimu kipindi cha Utawala wa Ukoloni wa Uingereza na hadi sasa yanaendelea kutumika.
Katika hatua nyingine Dkt. Christowaja Ntandu akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Bw. Achilles Bufure na Maafisa wa Idara ya Malikale amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Bw. Justus Kijazi kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja wa Uhifadhi wa maeneo ya Malikale kwenye Halmashauri hiyo.