Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga ameshauri kanuni za habari ambazo zipo njiani kutungwa ziangalie makosa ya kihabari ambayo yanaweza kutokea na kuyapatia ufumbuzi.
Dk. Henga ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha siku moja cha Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), kilichoitishwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).
Kikao hicho kililenga kupitia vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari vilivyopitishwa na bunge mwaka huu pia kuangalia mwelekeo wa Kanuni za Habari abazo zipo njiani kutungwa.
“Sera ya habari inayokuja, ipooze hili suala la wanahabari kuitwa wachochezi. Iondoe yale makosa ya jinai kwani suala la kupashana habari halipaswi kuwa na jinai ndani yake,” amesema.
Dk. Henga amesema, suala la kupashana habari ni haki ya kikatiba, na makosa yanaweza kutoka kama ilivyo kwa manaadamu yoyote hivyo, kufanya makosa hayo ya kitaaluma kuwa jinai, ni kuifinya tasnia ya habari.
“Katiba yetu Ibara ya 18 inasema, mtu ana haki ya kutoa, kupokea na kupata habari. Kanuni zitu zizipe ile mianya inayomtia mashaka mwanahabari,” amesema Dk. Henga.
Pia ameishauri serikali kuendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wanahabari kama ilivyo nia ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba, inawezekana sheria kurejeshwa bungeni kufanyiwa marekebisho hata kama haijaanza kutumika.
“Wito wangu, sheria haikatazi kufanya mabadiliko ya sheria mara kwa mara, kwa kuwa sheria ya habari bado ina kasoro, inaweza kupelekwa tena bungeni na kurekebishwa,” amesema.
Kwa upande wake Dk.Darius Mukiza kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari cha SMJC, alishauri mafunzo kuhusu sheria ya habari yanapaswa kutolewa vyuoni.
“Mambo yote kuhusu sheria ya habari yanapaswa kuingizwa kwenye vyuo vya habari, Kwani vijana wanatoka vyuoni wakiwa hawajui chochote kuhusu sheria hizi,” amesema Dk. Mukiza.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TEF, Neville Meena amesema, wanahabari wasio na sifa ya elimu inayohitajika katika tasnia ya habari, wanapaswa kushinikizwa kufanya hivyo kwa kuwa fursa ipo.
“Tutakua watu wa ajabu kama tutaendelea kukumbatia watu wasio na sifa kwenye tasnia ya habari, fursa ipo tuwahimize ili wawe na sifa,” amesema Meena.
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema, mchakato wa kutunga nanuni za habari unakaribia kuiva, hivyo ameishauri serikali kukutana na wadau wa habari na kupitia kanuni hizo kabla ya kuanza kutumika.