Na Shamimu Nyaki – WUSM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo chini ya Makamu Mwenyekiti Mhe. Ramadhan Suleiman Ramadhan leo Agosti 23, 2023 imepokea na kujadili taarifa ya Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Tanzania, kuhusu kuanzishwa kwa kampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha kwa kazi za Wabunifu.
Akizungumza katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti Mhe. Ramadhan ameipongeza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa kuanzisha Kampuni binafsi za Wabunifu za kukusanya na kugawa Mirabaha ambazo zitasaidia Wabunifu wa kazi za Sanaa na kazi za Maandishi kunufaika zaidi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ameieleza Kamati hiyo kuwa, Kampuni hizo zitakua na jukumu la Kukusanya na kugawa Mirabaha kwa wasanii ambapo Ofisi ya Hakimiliki itabaki kuwa msimamizi wa utekekezaji kwa Kampuni hizo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa COSOTA Bi. Doreen Sinare amesema kupitia CMO’S hizo Kampuni za nje zitakusanya mirabaha ya wabunifu wa hapa nchini pia zitakusanya mirabaha ya wasanii wa nje na baadaye kubadilishana makusanyo ili kugawa kwa wabunifu.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara imeelezwa kuwa Julai 21, 2023 COSOTA ilitoa Leseni ya Kukusanya na Kugawa Mirabaha kwa daraja la kazi za Muziki kwa Kampuni ya Tanzania Music Rights Society (TAMRISO), hivyo Kampuni hiyo itahitajika kuunda kanuni zake za viwango vya makusanyo ya leseni (mirabaha) kupitia wajumbe wake na kanuni hizo zitapitishwa na COSOTA kwa ajili ya utekelezaji.