Na. WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema itaendelea kushirikiana na Shirika la USAID kutoka nchini Marekani kwa kutoa mafunzo ya uelewa kwa wahudumu wa afya ngazi ya msingi ili kusaidia jamii kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya yanadumu na kuongezeka maradufu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID nchini Tanzania, Bw. Craig Haart kwa niaba ya Waziri Ummy Mwalimu leo Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao Dkt. Magembe amepata kumweleza vipaumbele vya wizara ya afya kuwa ni kuboresha Huduma za afya hususani katika afya msingi.
Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kumshukuru kwa ufadhili wanaoutoa katika programu za UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu(TB), Afya ya mama na mtoto, Mpango wa uzazi.
Amesema kama nchi sasa sekta ya afya inapambana kuimarisha Huduma za afya ya mama na mtoto, chanjo, kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi kwa mama na watoto wachanga pamoja na magonjwa yasiyoyakuambukiza.
Naye Bw. Haart amemshukuru Dkt. Magembe kwa ukaribisho mzuri na kuhaidikushirikiana na wizara ya afya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yana dumu na kuleta tija kwa wananchi wake.
“Sisi kama USAID tuko tayari kushirikiana na wizara ya afya ili Huduma za afya ziboreshwe zaini na kuleta matokeo kwa wananchi”. Amesisitiza Bw. Haart.