Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Nolasco Kipanda akitoa neno la utangulizi wakati wa mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa “Centre for Learning on Evaluation and Results CLEAR-AA” kutoka Chuo cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini, Prof. Dugan Fraser akiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wadau ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na Tathmini watendaji wa Serikali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael (hayupo pichani) yanayofanyika jijini Dodoma.
*********************************
Na Happiness Shayo – Dodoma
Matumizi sahihi ya Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini Serikalini
yanaongeza uwajibikaji na kuboresha utendaji kazi wa viongozi na
watumishi wa umma nchini hivyo kuwa na mchango katika
maendeleo ya utumishi wa umma na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael kwa
niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro wakati akifungua mafunzo ya wadau
ya siku mbili yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Ufuatiliaji na
Tathmini watendaji wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Michael amesema, kutokana na umuhimu wa Mfumo wa
Ufuatiliaji na Tathmini katika kuboresha nidhamu ya utendaji kazi
Serikalini, kuna haja ya mfumo huo kuwepo kisheria ili utekelezwe
kwa mujibu wa sheria katika Taasisi zote za umma nchini, hivyo kikao
hiki kina jukumu la kutoa mapendekezo sahihi ya kutekeleza azma
hiyo.
Dkt. Michael amefafanua kuwa, pamoja na kuanzisha sehemu za
Ufuatiliaji na Tathmini kwenye Wizara, Idara Zinazojitegemea,
Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni muhimu
kwa viongozi wenye dhamana kuwa na utashi wa kisiasa katika
kujenga Mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuongeza
uwajibikaji serikalini.
Dkt. Michael ameongeza kuwa, Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini
unatakiwa umguse mtumishi mmoja mmoja na taasisi kwa ujumla
ambapo watumishi na taasisi hawana budi kuonyesha matokeo
chanya kulingana na rasilimali zilizopo na kwa upande mwingine,
wananchi wana haki ya kuiwajibisha Serikali kwa kuitaka ionyeshe
matokeo chanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa “Centre for Learning on
Evaluation and Results CLEAR-AA” kutoka Chuo cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini, Prof. Dugan Fraser amesema, kituo hicho kipo
tayari kushirikiana na Serikali katika kuwezesha matumizi sahihi ya
Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini yatakayosaidia kuboresha
uwajibikaji, utoaji wa huduma bora, kurahisisha upatikanaji wa taarifa
kwa wakati na kuimarisha Utawala Bora kwa ajili ya maendeleo ya
Taifa.
Aidha, Prof. Fraser amesikitishwa na baadhi ya watendaji
wanaotumia muda mrefu kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi
mbalimbali na kutoa taarifa za miradi hiyo kwa kuchelewa na
kusababisha taarifa zilizopatikana kutokuwa na mchango tarajiwa
katika kufanya maamuzi.
Prof. Fraser ameweka bayana kuwa nchi isiyotumia Mfumo wa
Ufuatiliaji na Tathmini katika utekelezaji wa miradi yake husababisha
kuwa na sera mbovu, wananchi kutopata haki ya kuishauri serikali au
kutoa maoni juu ya utekelezaji wa miradi, na serikali husika
kutekeleza programu za maendeleo bila ufanisi.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa
Kazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Bw. Nolasco Kipanda amesema kufanyika kwa semina
kunatokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kuwajengea uwezo
kiutendaji wataalamu wake wa ufuatiliaji na tathmini, hivyo
amewataka wataalamu hao kutumia fursa hiyo kuongeza ujuzi ili
wawe na tija kwa maendeleo ya taifa.
Semina hiyo ina lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa Ufuatiliaji
na Tathmini inahudhuriwa na wadau kutoka katika Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa, Mahakama, Bunge, Tanzania Evaluation Association (TanEA)
na washirika kutoka Afrika Kusini.