Timu ya mpira wa miguu ya kata ya Kirumba imefanikiwa kuifunga timu ya mpira wa miguu ya kata ya Ibungilo magoli matatu kwa moja mchezo uliochezwa katika uwanja wa Baptist Kona ya Bwiru wilayani Ilemela.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mchezo huo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Charles Karoli amezitaka timu hizo kutumia michezo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja kuibua vipaji na kukuza vile vilivyopo
‘.. Kwanza niwapongeze kwa utayari wenu katika kushiriki mashindano haya lakini niwaombe kuhakikisha tunatimiza malengo ya Mbunge Dkt Angeline Mabula katika kuanzisha mashindano haya kwa kuonyesha na kuibua vipaji ..’ Alisema
Aidha Ndugu Karoli amewahakikishia wanamichezo na wananchi Kwa ujumla kuwa Mbunge Dkt Angeline Mabula ataendelea kuunga mkono juhudi zote za kukuza michezo na vipaji ndani ya Jimbo lake hivyo kuwaasa kuendelea kumuunga mkono
Kwa upande wake nahodha wa timu ya kata ya Kirumba Edwin Fundikira amesema kuwa mafanikio ya timu yao yametokana na kufuata maelekezo ya mwalimu pamoja na kutambua umuhimu wa mchezo huo kwa timu yao sanjari na kuwaahidi mashabiki kuzidi kufanya vizuri katika michezo inayofuata
Nae mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM kata ya Ibungilo Ramadhan Fadhili ambae ndie msemaji wa timu ya kata yake mbali na kumshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula Kwa kuassisi mashindano hayo ameongeza kuwa timu yake imeshindwa kutamba katika mchezo huo kwa kuwa wachezaji wake bado hawajawa na muunganiko wa pamoja hivyo kuahidi kufanya vizuri katika mchezo unaofuata
Magoli ya timu ya kata ya Kirumba yamefungwa na mchezaji Mboba Japhet jezi nambari 15 huku la pili na la tatu yote yakifungwa na mchezaji Musa Asante jezi nambari 16 wakati timu ya kata ya Ibungilo ikiambulia goli moja pekee kutoka Kwa mchezaji Khamis Jafar jezi nambari 10.