Wananchi waliovamia Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wakitii agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kubomoa majengo na vibanda vyao ili kuacha wazi eneo la Mpaka huo.
Zaidi ya asilimia 80 ya Wananchi waliovamia Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma wametii agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kubomoa majengo na vibanda vyao ili kuacha Mpaka wazi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo la Rais na kukuta wananchi wametii na wamebomoa.
“Ninawapongeza wananchi wa Tunduma kwakuwa wameitikia agizo la Rais na utekelezaji unakwenda vizuri sana, nyumba na vibanda vingi vimebomolewa na watu wanahamisha bidhaa na vifaa ambavyo watavitumia wakienda sehemu nyingine, hivyo ninawapongeza sana kwa Mwitikio mzuri.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa kutokana na kuridhishwa na kasi ya kubomoa ameamua kuwaongezea siku tatu ambazo zitatumika kumalizia kuhamisha bidhaa na vifaa kutoka katika eneo la mpaka na baada ya hapo chochote kitakachobaki hapo kitabomolewa na serikali.
Brig. Jen. Mwangela amesema wananchi waliobaki wanapaswa kuondoka na kuacha Mpaka wazi kwakuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwenye mipaka waweze kutekeleza majukumu yao bila bila kukwamishwa na kituo pia hakutaruhusiwa shughuli za biashara katika eneo la Mpaka.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando amesema Jeshi la Polisi limerahisishiwa namna ya kupambana na uhalifu na kuzuia Magendo kutokana na kushafishwa eneo la mpaka.
Kyando amesema anampongeza Rais Magufuli kwa amri ya kusafisha mpaka huo kwani hali ya amani itazidi kuimarika katika eneo hilo na pia ameshuhudia zoezi la kubomoa likifanyika kwa amani.
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Songwe Philon Kyetema amesema kabla ya usafishaji wa Mpaka, zoezi la kupambana na wahamiaji haramu lilikuwa gumu kwakuwa walikuwa wanaweza kuingia na kutoka nchi jirani kwa urahisi kupitia vichochoro.
Amesema Wananchi wa Tunduma wategemee hali kuimarika Zaidi kwakuwa sasa wataweza kufanya ukaguzi wakati wote na kwa kutumia njia mbalimbali kama magari pikipiki na hata kwa miguu kwakuwa wamerahisishiwa mazingira ya kufanyia kazi.