Mkuu wa wilaya ya Mbulu Komredi Kheri James, mapema leo amepokea Ujumbe wa Maafisa na Wataalamu kutoka wizara ya Ujenzi na TANROARDS Makao, waliofika Wilaya ya Mbulu kwa lengo la kumtambulisha Mkandarasi na kumuonesha maeneo ya mradi huo, pamoja na kutoa Taarifa rasmi ya kuanza kwa Ujenzi wa Barabara hiyo Muhimu.
Akizungumza katika kikao kazi na ujumbe huo kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, KomredI Kheri James kwa niaba ya Wananchi, Viongozi na watumishi wa Wilaya ya Mbulu, Amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Uamuzi Makini wa Kujenga Barabara hiyo.
Komredi Kheri James ameeleza kuwa ujenzi wa Barabara hiyo utafungua uchumi wa Wananchi Mbulu, utarahisisha mawasiliano na kuchochea biashara baina ya wilaya ya Mbulu na maeneo mengine.
Akizungumza na Wananchi katika eneo la Stendi ya Mbulu kwa lengo la kuwapa taarifa rasmi ya kuanza kwa Mradi huo, Komredi Kheri James amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi katika maeneo yote yatakayo pitiwa na mradi huo, lakini pia amewasihi wananchi kuutazama Ujenzi huo kama fursa ya kichumi kwa kwa kupata kazi na kuuza huduma katika kipindi chote cha Ujenzi.
Aidha Komredi Kheri James amemhakikishia ushirikiano Mkandarasi na TANROARDS , katika suala la Usalama na hatua zote za kuanza na kutekeleza Mradi huo ili uweze kuanza kwa wakati na kukamilika kwa wakati ukiwa na ubora uliokusudiwa.
Kuanza kwa ujenzi wa Barabara hii ni ufunguo wa dhahabu katika mlango wa mafanikio ya Wananchi wa Mbulu.