Rombo. Na Ashrack Miraji
Watendaji na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kuendelea kushirikiana na kushirikisha jamii katika kukamilisha miradi ya maendeleo sambamba na kutatua kero zinazowakabili wananchi kwenye maeneo yao.
Hayo yamesemwa na katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro,Tixon Nzunda wakati akizungumza na watumishi hao baada ya kutembelea miradi ya maendeleo wilayani humo ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Cha Kisale.
Nzunda amewahimiza viongozi hao kushirikisha wananchi katika ukamilishaji wa miradi hiyo ukiwemo wa Zahanati ya Kijiji hususani kusafisha eneo hilo ili huduma zitakapoanza kutolewa iwe rahisi kuwahudumia.
Pia amepongeza jitihada zinazofanywa na Mkuu wa Wilaya hiyo ya Rombo kanali Hamis Maiga, Mkurugenzi Godwin Chacha pamoja na timu yake kwa kusimamia na kuhakikisha ubora wa miradi unaendana na thamani ya fedha zinazotolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. .Samia Suluhu Hassan.
Miradi aliyotembelea na kukagua katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rombo, ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kisale,madarasa matatu na ofisi moja shule ya msingi Useri na madarasa na bweni shule ya sekondari ya Kutwa ya Tarakea.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamis Maiga amemshukuru katika tawala huku akiahidi kutekeleza maelekezo aliyotoa ili wananchi wapate huduma stahiki kupitia miradi inayotekelezwa na serikali.