Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mkoa wa Dodoma, Eng. Grayson Maleko (kulia), alipokagua maendeleo ya karakana ya Wakala huo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mkoa wa Dodoma, Eng. Grayson Maleko (kulia), kuhusu kuhamisha magari chakavu yaliyotelekezwa, alipokagua maendeleo ya karakana ya Wakala huo Jijini Dodoma.
Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa wa Dodoma, Eng. Grayson Maleko (kulia), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya (katikati), alipokagua maendeleo ya karakana ya Wakala huo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akizungumza na mafundi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mkoa wa Dodoma alipokagua maendeleo ya karakana ya Wakala huo Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu, alipokagua maabara ya vifaa vya wakala huo jijini Dodoma.
……….
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya amezitaka Taasisi za Wakala wa Barabara (TANROADS) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani Dodoma kuweka mikakati ya kufanya kazi kitaifa badala ya kufanya kazi kimkoa kama ilivyokuwa awali.
Akizungumza alipokagua karakana ya TEMESA Mkoa wa Dodoma na maabara ya kupima vifaa vya ujenzi ya TANROADS, mkoani humo Naibu Waziri Kasekenya, amehimiza kuwa ni vyema taasisi hizo zikajiimarisha kuhudumia watu wengi waliohamia katika makoa makuu ya nchi kwa kuboresa idadi ya wataalamu, vifaa na kufanya kazi zenye ubora kwa muda mfupi.
“TEMESA himizeni ubunifu na uadilifu kwa watumishi wenu ili Taasisi nyingi na watu binafsi wavutiwe kutengeneza magari yao katika karakana yenu na kunufaika na utaalamu wa huduma nyingine za masuala ya umeme mnazotoa”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Amezungumzia umuhimu wa TEMESA kuwaelimisha wateja wao umuhimu wa kuondoa magari mabovu yaliyotelekezwa katika karakana hizo ili kupata nafasi ya kutosha kuhudumia idadi kubwa ya magari inayohudumiwa na karakana hiyo.
Aidha, amezitaka TEMESA na TANROADS kuendelea kutoa fursa kwa wanafunzi wenye taaluma ya uhandisi kufanya mazoezi ya vitendo ili kuwajengea uwezo vijana wengi zaidi na kuwafundisha ubunifu.Kwa upande wake, Meneja wa TEMESA mkoa wa Dodoma, Eng. Grayson Maleko, amemuomba Naibu Waziri huyo kusaidia Taasisi hiyo kupata watumishi wa kutosha ili kuongeza tija na kuwezesha kufikia malengo waliyojiwekea.
Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Eng. Leonard Chimagu, amemhakikishia Naibu Waziri kuwa TANROADS imejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inayoendelea jijini Dodoma inasimamiwa kikamilifu na kukamilka kwa wakati.
Naibu Waziri Kasekenya, alikuwa katika ziara ya kukagua utendaji wa TEMESA na TANROADS ili kujionea namna taasisi hizo zinavyoendana na mabadiliko na kuhudumia idadi kubwa ya watu kwa kuwa katika makao makuu ya nchi.