Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na UKIMWI kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 04 hadi 08 Novemba 2019,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya Mkutano huo kulia ni Dkt. Leonard Subi Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia, Wazee, na Watoto.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo Zamaradi Kawawa akoa ufafanuzi masuala kadhaa katika mkutano huo.
Baadhi ya wataalam kutoka wizara ya Afya na Tume ya Kudhibiti Ukimwi TACAIDS wakiwa katika mkutano huo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya Mkutano huo kushoto ni Dkt. Zainad Chaula Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
…………………………………………………
Na John Bukuku
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na UKIMWI kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 04 hadi 08 Novemba 2019.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya mkutano huo kwenye ukumbi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) jijini Dar es salaam leo.
Waziri Ummy Mwalimu amesema Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na UKIMWI unatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na UKIMWI unalenga kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC ya mwaka 1999 na Mpango Mkakati wa Kanda kuhusu masuala ya Afya pamoja na kuridhia kwa pamoja maazimio mbalimbali kuhusu masuala ya afya kwa nchi za SADC.
“Agenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni Magonjwa ya kuambukiza yanayoziathiri nchi za SADC kama vile Kifua Kikuu, Malaria na UKIMWI, Masuala ya lishe na Uimarishaji wa Mifumo ya Afya” Amesema Ummy Mwalimu.
Ameongeza kuwa Bado nchi zote kumi na sita zina changamoto za maambukizi ya UKIMWI,Tanzania tumeweza kupunguza maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017 na bado juhudi za kuchukua hatua ili kupunguza zaidi maambikuzi ya UKIMWI zinaendelea.
Kwa upande wa ugonjwa wa kifua kikuu Kidunia nchi thelathini zinazobeba mzigo mkubwa wa Kifua Kikuu(TB),Tanzania ipo katika nchi tano kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinazokabiliwa na ugonjwa huu.
Tanzania imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi 10 zilizofanikiwa katika kuwaibua wahisiwa wa ugonjwa wa TB, ambapo Mgonjwa wa TB akitumia dawa vizuri anapona.