Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bw. Ismail Seleman akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 16/8/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji katika kipindi Cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni 2023.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia miradi tisa yenye thamani ya Sh. 72, 396, 802, 813 . 39 pamoja na kubaini mapungufu kwa baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Mabwepande ambapo msimamizi wa mradi hakuna na sifa na vigezo na kusababisha kutekeleza chini ya kiwango.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 16/8/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni 23, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni Bw. Ismail Seleman, amesema kuwa msimamizi wa mradi wa Zahanati Mabwepande wenye thamani ya Shilingi 268,980, 424.34 anaendelea kuzunguzwa.
Bw. Seleman amesema kuwa miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa madarasa 12 ya Sekondari Boko Mtambani wenye thamani ya Sh. 650,000,000 ambapo umeshindwa kukamilika kwa wakati kutokana na ucheleweshaji wa fedha kutoka katika vyanzo.
“Pia Kuna ujenzi wa Mabweni matano umeshindwa kukamilika kwa sababu mkandarasi wa kwanza alisaini BOQ ya bweni moja badala ya matano ilivyokuwa kwenye tangazo la zabuni na hivyo kusababisha gharama kubwa hali iliyopelekea malengo kutokukamilika” amesema Bw. Bw. Seleman.
Bw. Seleman amesema kuwa wamepokea malalamiko 48 yaliyohusu vitendo vya rushwa ikiwemo madai, dhuluma, kughushi, kutapeli, mikopo umiza pamoja na kutoridhishwa na kesi Mahakamani.
“Tumeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia semina katika maeneo tofauti ikiwemo taasisi za serikali na sekta binafsi, mkutano wa hadhara katika kata za Mbweni, Mbezi Juu, Mzimuni, Kijitonyama, Wazo, Mikocheni, Kinondoni, Msasani, Kigogo na Tandale” amesema Bw. Seleman.
Amefafanua kuwa wameendelea kuimarisha klabu za kupinga vitendo vya rushwa katika Shule ya Sekondari Feza Girls, shule ya msingi Mabwepande pamoja na kuendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari.
“Katika kipindi hiki tumezifikia Kata 5 ambapo kupitia vikao na wadau, kero 25 ziliibuliwa na kati yake tayari kero 19 zimeshapatiwa ufumbuzi” amesema Bw. Seleman.
Bw. Seleman amewasihi wananchi wote waendelee kutoa taarifa zozote kuhusu rushwa na utapeli Kwa kutoa taarifa kupitia mitandao ya simu kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa namba ya dharula 113.