Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera ameongoza mazishi ya mzee wa miaka 93 Maliake Laizer yaliyofanyika kijiji cha Naisinyai.
Marehemu mzee Maliake kwenye kizazi chake amejaliwa kupata uzao wa watu 307 wakiwemo watoto 41, wajukuu 219, vitukuu 45 na vilembwe wawili.
Akizungumza kwenye mazishi hayo Dk Serera amewapa pole wakazi wa kata ya Naisinyai kwa kuondokewa na mzee Maliake.
“Tulikuwa na ziara ya kamati ya siasa ya wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa wilaya Kiria Laizer ndipo tukafika kuhani ili baadaye tuendelee na ziara yetu,” amesema Dk Serera.
Katibu mwenezi wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Mosses Makeseni akisoma historia ya marehemu Maliake amesema amezaliwa mwaka 1930 kwenye kijiji cha Lorbene kata ya Naberera.
Makesema amesema wakati wa uhai wake mzee Maliake alikuwa anajishughulisha na ufugaji na kilimo cha kujikimu.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema marehemu Maliake ambaye ni muasisi wa chama chao alikuwa mtu mwema mwenye kupenda haki na asiyeonea mtu.
“Hata kifo chake kimetokea bila kuteseka kwani walikuwa wanakula nyama naye akawagawia baadhi ya wageni alipomaliza akatoa taarifa kuwa anaumwa akapelekwa zahanati ya Moipo Mirerani kisha akafariki dunia,” amesema Ole Sendeka.
Mtoto wa marehemu huyo mchungaji Joshua Maliake amesema baba yake alioa wake wanne na mke mmoja alipofariki alioa mwingine ili kutimiza tena idadi ya wake wanne.
“Tumepanga baada ya mazishi kesho yake tukutane kwani ndugu tupo wengi na hatujuani wote, hivyo tutakutana tuwatambue ndugu wa baba wadogo na baba wakubwa,” amesema Joshua