Mashindano ya mpira wa miguu kwa timu za wanaume na wanawake kutoka kata 19 za Jimbo la Ilemela na kisiwa cha Bezi maarufu kwa jina la The Angeline Jimbo Cup 2023 yaliyoasisiwa na mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula yamekuja na ubunifu wa tofauti ili kuyafanya kuwa bora zaidi.
Akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya mashindano hayo kwa mwaka wa 2023 kilichofanyika katika ukumbi wa uwanja wa CCM Kirumba, Katibu wa ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Charles David amesema kuwa kwa mwaka huu mashindano yamehusisha wataalam kutoka ofisi za manispaa na watendaji wa kata, viongozi wa chama cha michezo wilaya ya Ilemela na wataalam wake na viongozi wa CCM ngazi za kata na wilaya ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa la kuibua vipaji na kuendeleza vipya linafikiwa
Angeline Jimbo Cup 2023 limehusisha makundi mbalimbali ya Serikali, Chama Cha Mpira wa miguu wilaya ya Ilemela IDFA, Chama Cha Mapinduzi na jumuiya yake ya Uvccm ili kuongeza tija ya kuanzishwa kwake ..’ Alisema
Aidha Ndugu David ameongeza kuwa kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zimeibuliwa katika msimu uliopita zimekwishafanyiwa kazi hivyo kuwatoa hofu washiriki pamoja na kusisitiza umoja na mshikamano wakati wote wa mashindano.
Nae katibu wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Ilemela IDFA Ndugu Almas Moshi Almas amesema kuwa mashindano ya The Angeline Jimbo Cup 2023 yamekuja na taratibu mpya kwa lengo la kuongeza ufanisi ikiwemo kuzuia kuchezesha wachezaji wa nje ya wilaya ya Ilemela, kutumia utaratibu wa fomu ya usajili wa wachezaji watakaoshiriki mashindano ili kuzuia kuchezesha mamluki, kusajili wachezaji kwa kutumia kadi maalum zenye taarifa muhimu za wachezaji pamoja na kutumia makocha na marefa wenye vigezo na wanaotambulika na Chama Cha Mpira wilaya ya Ilemela.
Kwa upande wake katibu wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM wilaya ya Ilemela (UVCCM) Ndugu Magohe Hamis amemshukuru na kumpongeza mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kushirikisha chama na jumuiya hiyo moja kwa moja utaratibu unaotoa fursa ya ushiriki wa vijana walio wanachama na wasiowanachama kwa usawa.
Maarufu Mohamed ni mtendaji wa kata ya Pasiansi ambapo amepongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kuanzisha mashindano hayo sanjari na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano huo katika maeneo yao pamoja na kuahidi kuisimamia timu yake kwa kushirikiana na wadau wengine ili iweze kuibuka mashindi wa mashindano hayo na kuchukua kombe kwa msimu wa mwaka huu wa 2023.