Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu akizungumza na waandishi wa habari Leo jijini Dar es Salaam kuhusu kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi za taasisi za Umma na wakuu wa mashirika hayo kitakachofanyika jijini Arusha kuanzia Agosti 19 na kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la wakuu wa Taasisi za Umma ambaye pia ni Mkurugenzi mkuu wa TANTRADE Bi.Latifa Khamis akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Leo jijini Dar es Salaam.
…………………………………
*Ofisi ya Msajili imejipanga kubadili fikra na utendaji kazi
*Taasisi ziko tayari kushiriki, Rais Samia Suluhu Hassan Mgeni Rasmi
Na Beatrice Sanga-MAELEZO
Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema itahakikisha inasimamia mabadiliko na mageuzi mbalimbali katika Taasisi, Mashirika ya Umma, Wakala za serikali pamoja na Kampuni na Taasisi ambazo zina ushirikiano/ubia na serikali ili kuhakikisha kuwa shughuli za uchumi na maendeleo ya Taifa na wananchi kwa ujumla zinakwenda kwa kasi na kwa ufanisi zaidi.
Hayo yamesemwa August 13, 2023 na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea juu ya Kikao Kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi (CEOs Forum) ambacho kitafanyika kuanzia August 19 hadi 21, Jijini Arusha katika Kituo cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kitakachowakutanisha Wenyeviti na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali ili kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya mifumo, Sheria na kutoa mwelekeo mpya wa utendaji kazi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili.
Mchechu amesema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Kikao Kazi hicho ambacho mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na kukumbushana majukumu ya kila mmoja katika Taasisi hizo, Kujengeana uwezo kiutawala, na Teknolojia, Maboresho ya usimamizi wa Taasisi na vigezo vya utendaji kazi, Kupitia na kujadili Dira ya Maendeleo ya Taifa, kujadili changamoto za kiutendaji katika Taasisi hizo na mkakati wa kuzitatua katika Taasisi pamoja na mafunzo mbalimbali ya uongozi ili kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo.
“Tutakuwa na utambuzi wa baadhi ya Taasisi ambazo zimefanya vizuri, kutakuwa na utambuzi na zawadi shughuli ambayo itafanywa na Rais Samia, tumeweka utambuzi huo katika vipengele vinne, kigezo cha kwanza Taasisi zinazochangia gawio, pili, Taasisi ambazo serikali ina hisa chache, ambazo zimechangia gawio kubwa serikalini, lakini pia Taasisi zisizo za kibiashara, na Taasisi zilizozalisha faida nyingi, na kipengele cha kampuni zilizobadilika zaidi kiutendaji (a most transformed company) maana kuna kampuni tulikuwa tunatamani tuzifute kabisa lakini kwa sasa zimebadili sana, tutaenda kuzitambua na hii ni katika kuleta ushindani na uwazi ndani ya Taasisi zetu,” amesema Mchechu na kuongeza,
“Mwaka huu tunahusika na yaliyo mazuri, hatukutaka kuviziana kwa yaliyo mabaya, kwasababu watu wangesema hawakuajiandaa lakini miaka ijayo nafikiri tutakuwa na koti jeusi, wale ambao wanazalisha chini ya kiwango kabisa tutaenda kuwatambua nao.”
Mchechu amesema kuwa Kikao Kazi hicho kitakuja na dira mpya ya utendaji kazi na uzalishaji na hivyo kuongeza ufanisi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Taasisi za Umma na Taasisi zao.
“Naamini kuwa baada ya kikao hicho tutaenda kuona mabadiliko makubwa katika Taasisi zetu kwa mwaka ujao, malengo yetu ni mabadiliko nafikiri kabisa kufikia 2030 tutakuwa na Taasisi zilizobadilika, tupo katika mabadiliko tunaenda kuanza pamoja kwenye kikao chetu, sisi tukiamka ndiyo tutakuwa tumebadili uchumi wa nchi,” amesema Mchechu.
Mchechu amesema katika Kikao Kazi hicho, ofisi yake imejizatiti kuhakikisha inasimamia R4 za Rais Samia ambazo ni Maridhiano (Reconciliation), Mabadiliko (Reforms) Ustahimilivu (Resilience) pamoja na Kujenga Upya (Rebuilding) ili kuhakikisha kuwa Taasisi, Wakala na Mashirika yanabadilisha mtazamo wake kiutendaji na katika uzalishaji mali, aidha amesema Kikao Kazi hicho kitajadili namna ya kuboresha uhuru wa Taasisi hizo ili ziwe na ufanisi katika kusimamia rasilimali za nchi kwa maslahi ya watu wote.
“Baadhi ya Taasisi tutaangalia sheria zao ambazo labda zimepitwa na wakati zinatakiwa ziboreshwe, tutaenda kuimarisha namna ya kupata viongozi wa Taasisi hizo ili kuwa na viongozi wenye uwezo na utalaam kuzisimamia hizo Taasisi, namna ya kuchaguliwa kwa bodi za Wakurugenzi, tutakuwa tunaajiri kwa kuangalia changamoto ambazo Taasisi zake zinapitia.” amesema Mchechu.
Hata hivyo Mchechu amesema kuwa watahakikisha kikao kazi hicho kinatoa mwelekeo mzuri hususani kwa Taasisi ambazo bado zinaitegemea serikali kuu katika bajeti zao za kila mwaka na uendeshaji wa shughuli zake, ili kuhakikisha kuwa pesa ambazo zinatumiwa ziende kuhudumia mambo mengine.
“Tuna Taasisi chache ambazo siwezi kuzitaja leo ambazo wakati mwingine bado zimekuwa zikipata msaada kutoka serikalini, hawa tunaenda kukumbusha nao vizuri Arusha, nafikiri wana mwaka mmoja na wale ambao wana changamoto kubwa zaidi hawa tunaweza kuwaruhusu kwa mwaka mwingine wa pili, ambao watakuwa wanafanya mabadiliko na ujenzi mpya katika taasisi zao, vinginevyo hakuna sababu mna bodi, mna rasilimali watu, na mna menejiment halafu bado mnaendelea kulipiwa na serikali.”
Kwa upande wake Latifa Khamis Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) amesema kuwa kikao kazi hicho kitasaidia kupunguza malumbano mbalimbali ambayo yamekuwa yakitokea katika Taasisi mbalimbali na hivyo kitaongeza utendaji kazi na ufanisi.
“Jukwaa letu hili, malengo yake makubwa ni kurahisisha mawasiliano baina yetu ili kufanya utekelezaji wa majukumu yetu uwe rahisi, badala ya kuhangaika kumtafuta mwenzako kwa njia mbalimbali, lakini jukwaa letu litatusaidia kukusanyika pamoja ili tuweze kusaidiana katika kufanikisha utekelezaji wa malengo yetu.”
Kikao Kazi hicho ni cha kwanza ambacho kitawakutanisha Wenyeviti, Wakurugenzi, Watendaji wa Taasisi, Wakala za serikali, Mashirika ya Umma 248 zilizopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, pamoja na Taasisi 302 ambazo Serikali ina ubia nazo.