Bohari ya Dawa (MSD), imeingia mkataba na kampuni ya Hainnan International kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kisasa (WiB) yenye ukubwa wa sqm elfu 5, kwa ajili ya uhifadhi wa bidhaaa za afya, Kanda ya MSD Dodoma.
Maghala haya yatakua kitovu (hub) cha uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya kwenye Kanda nyingine za MSD hasa zinazohudumia Kanda ya Kati, Kanda ya Magaharibi, na Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mradi huo, Meneja Miradi wa MSD, Deo Orauya amesema kuwa, kutokana na ongezeko la watu na ujenzi vituo vipya vya kutolea huduma za afya nchini, MSD imejidhatiti kuongeza uwezo wake wa uhifadhi, ili kuendana na mabadiliko hayo kwa kujenga maghala ya kisasa, ambapo pia utasaidia uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya nchini.
Aidha ameongeza kwamba zoezi la makabidhiano ya eneo la ujenzi, yameongozwa na mshauri mwelekezi Architect Nkini kutoka kampuni ya ABECC, inayomilikiwa na chuo kikuu cha Ardhi -Dar es Salaam.
Ujenzi wa maghala haya yenye ukubwa wa sqm elfu 5, katika kiwanja na.92/1&2/Kizota Dodoma, jirani na Ofisi za Kanda za MSD, unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 10, huku ikiakisiwa kwamba utakamilika ndani ya muda mfupi zaidi.