Wawakilishi wanne walioteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika hatua ya awali ya Shindano la Future Face Kimataifa 2023 wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kutangazwa kushinda usahili uliohusisha vijana zaidi ya 200 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
………………….
Na Mwandishi Wetu
WANAMITINDO wanne kati ya 200 waliojitokeza kwenye usahili wa Shindano la Future Face 2023 wameteuliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye chaguo la awali la Future Face duniani 2023.
Usahili wa Shindano hilo la Future Face umefanyika kwa kushirikiana na kuratibiwa na Mwanamitindo wa kimataifa Millen Happiness Magese umefanyika jijini Dar es Salaam huku majaji wa nne wakihusika katika kuchuja wanamitindo waliojitokeza hadi kubakia na wawakilishi wanne kati ya hao 200 waliojitokeza.
Majaji katika usahili wa shindano hilo la kimataifa ambalo ndio mara ya kwanza kufanyika nchini Tanzania walikuwa Ally Rehmtullah, Mwanamitindo wa Kimataifa Millen Happiness Magese, Martin Kadinda na Jamilla Vera Swai.
Akitangaza matokeo ya usahili huo Mwanamitindo wa Kimataifa Millen Happiness Magese amesema kuwa vijana zaidi ya 200 walitokeza kwenye usahili uliofanyika mwishoni mwa wiki lakini baada ya kuangalia sifa na vigezo vya Shindano hilo wamefanikiwa kuwapata wawakilishi wa nne ambao hao watachuana tena na kumpata mmoja ambaye ataiwakilisha nchi ya Tanzania katika mashindano hayo.
Amewataja walioteuliwa kwenye usahili huo ni Rachel Amani Julius(20) – 5’8 Ft, Joyceller Lasway(25l – 5’9 Ft, Neema Evaresty(23) – 5’11 Ft pamoja na Jasinta David Makwabe(25) – 5’11 Ft.
Mwanamitindo wa Kimataifa Millen Happiness Magese amesema baada ya kupatikana kwa wawakilishi hao hakutakuwa na kambi huku akifafanua yule atakayechaguliwa kuiwakilisha nchi Septemba mwaka huu atakwenda nchini na Nigeria na akifanikiwa kushinda anakwenda nchini Paris au Italy.
“Nawashukuru majaji wote kwa ushiriki na kujitoa kwao kufanikisha jambo hili muhimu ambalo limeandika historia kubwa katika nchi yetu kwani ndio mara ya kwanza Shindano la Future Face linafanyika nchini Tanzania.
” Pia nawashukuru sana vijana wote kwa kujitokeza kwa wingi, sikutegemea kuona umati uliojitokeza na Kama mtu hakuweza kufika basi anaruhusiwa kutuma maomba yake kwa njia ya mtandao kupitia www.futurefaceglobal.com ambapo mwisho ni Septemba 22, 2023″ amesema.
Aidha amevishukuru vyombo vya habari nchini Tanzanka kwa kuendelea kutoa ushirikiano hasa katika kuripoti kuhusu shindano hilo la kimataifa kila hatua inayofanyika ikiwemo ya usahili huo.
Kuhusu walioteuliwa amesema wawe washindani kwamba wakubali kushinda au kushindwa. Pia kushindwa waichukulie kama sehemu yao kuendelea kujaribu tena hasa kwa kutambua mashindano hayo ni makubwa na yanaangaliwa na mamilioni ya watu duniani kote.
Awali wakati anazungumzia Shindano hilo, Mwanamitindo wa Kimataifa Millen Happiness Magese amesema ameshirikiana na Future Face kuleta Shindano hilo kubwa zaidi la kimataifa la kusaka wanamitindo mwaka wa 2023.
Amesema Shindano hilo ni la kipekee lililoandaliwa na Wakala mkubwa zaidi wa wanamitindo barani Afrika, Beth Model Management na limekuwa linajivunia utofauti wake wa ukubwa, umri, rangi na kabila, na ulemavu, huku shindano likiwa na sera ya fursa sawa.