Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar Yassir Ameir Juma akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na mfuko wa huduma za Afya unaotarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwaka huu wakati wakipatiwa mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya huduma hiyo.PICHA NA FUAZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya mfuko wa huduma za Afya Zanzibar ambao unatarajiwa kuanza kutumika mwezi ujao.PICHA NA FUAZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR.
…………
Na Rahma Khamisi, Maelezo Zanzibar
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar Yassir Ameir Juma amewataka wafanyakazi wote na wananchi kujiunga na mfuko wa huduma za afya ZHIF ili kupata huduma bora zaidi nchini.
Akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuanzishwa kwa Mfuko huo huko Michezani Mall amesema mfuko huo utawasaidia wananchi wote bila ya kujali rangi wala kabila .
Amesema lengo la mafunzo hayo kwa Waandishi ni kuhakikisha wanakuwa na uelewa kuweza kuelimisha na kushajihisha wananachi kutambua dhamira ya mfuko huo namna utavyowafikia na kuwanufaisha.
“Tunafanya mafunzo haya kwenu nyinyi ili mufikishie taarifa kwa jamii waweze kufahamu dhana na faida ya mfuko huo na kuweza kujiunga kwa maslahi ya afya na Taifa kwa ujumla.
Aidha amefahamisha kuwa mfuko huo utawasaidia wananchi wote kupata huduma za msingi bila ya kujali vipato vyao na ni msaada zaidi kwa wananchi wa kipato cha chini ambao hawamudu gharama za matibabu makubwa.
Katika hatua nyenine Mkurugenzi Mkuu amefafanua kuwa kwa wafanyakazi makato yatakua ni silimia 7 ambapo asilimia hizo zitachangiwa kwa mgao sawa kati ya mwajiri na mwajiriwa .
Aidha aliishauri jamii kuachana na taarifa zizsizo sahihi zinazopelekea kuwa na dhana potofu juu ya mfuko huo na kuwataka kushirikiana katika hilo ili kuleta mageuzi makubwa ya Afya Visiwani.
Mapema Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidhi akifungua mafunzo hayo amesema lengo la Serikali kuanzisha Mfuko huo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya chini.
Amesema mfuko huo utawasaidia wananchi wa kipato cha chini kupunguza gharama za kufuata matibabu nje ya nchi hasa maradhi makubwa ikiwemo matibabu ya Saratani ,Figo na huduma za kibingwa.
Aidha amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti iliofanywa asilimia 25.6 ya wananchi hawataweza kuchangia mfuko huo hivyo Serikali itawachangia ili wapate huduma bora za afya.
Aidha amefahamisha kuwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepitisha sheria No 1 ya mwaka 2023 juu ya dhana ya mfuko wa huduma za afya kwa wananchi ili waweze kupata huduma bora zaidi.
Naibu Waziri ameeleza kuwa mfuko huo ili uanze kufanya kazi lazima uchangiwe ambapo kwa kuanzia utaanza na wafanyakazi wa Serikali na baadae Sekta binafsi hadi kuwafikia wananchi wote wa Zanzibar
“kuna kila sababu ya kujipanga na kubuni miundombinu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya kwa kuanzisha Mfuko wa huduma bora ya afya ili kupata matibabu bora nchini ” alifahamisha Naibu Waziri.
Amefahamisha kuwa Serikali inapoteza fedha nyingi kuwapeleka Wananchi wake nje ya Nchi kwaajili ya matibabu hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo kutasaidia kuzuwia upotevu wa fedha hizo.
Nao washiriki wa semina hiyo wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwafahamisha wananchi kuhusu mfuko huo ili kuondosha dhana potofu miongoni mwa jamii.
Mfuko wa Huduma za Afya kwa Wote unatarajiwa kuanza kutumika mapema Oktoba Mwaka huu.