NA JOHN BUKUKU, MBEYA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limejipanga kuendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi katika kutoa huduma
kwa ufanisi ikiwemo kufanya uchunguzi wa vyombo vinavyosafirisha abiria, bidhaa mbalimbali majini.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima Nanenane kwenye Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge, amesema kuwa shirika linaendelea kutoa elimu kwa wananchi waweze kujua linatoa mchango gani katika kuboresha uchumi nchi na kufikia malengo tarajiwa.
Bw. Mkeyenge amesema kuwa Mkoa wa Mbeya upo kimkakati ambao unazalisha mazao mbalimbali ikiwemo mchele na Maharage ambapo wakati mwengine wanatumia usafiri wa majini katika kusafirisha mazao.
“Tunaendelea kudhibiti usafiri wa vyombo vya majini ambao unaendana na viwango vya Kimataifa katika kutoa huduma” amesema Bw. Mkeyenge.
Bw. Mkeyenge amefafanua kuwa Mkoa wa Mbeya kuna ziwa Nyansa ambapo kuna vyombo vinavyofanya safari zake ikiwemo kusafirisha mizigo na abiria hadi nchi ya Malawi.
“Shirika lipo kuhakikisha viwango vya usafiri vinaendana na viwango katika kuleta tija hapa nchini, natoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya majini katika Ziwa Nyansa kufata sheria na utaratibu” amesema
Bw. Mkeyenge.