Happy Lazaro , Arusha.
Idadi ya watalii walioingia nchini kipindi cha januari hadi juni 2023 imezidi kuongezeka mara dufu hadi kufikia 759,327 huku wengi wakitokea nje ya bara la Afrika.
Mkurugenzi mkuu wa takwimu za kiuchumi nchini, Daniel Masolwa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Amesema kuwa ongezeko hilo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya watalii 575,397 walioingia kipindi kama hicho mwaka 2022 ambayo ni sawa na asilimia 31.9.
“Watalii wengi zaidi walitoka Marekani ambao ni 51,674, wakifuatiwa na Ufaransa 48,696 na Ujerumani waliokuja 39, 789 huku Uingereza na italia wakija 29,000”
Amesema kuwa watalii wa Afrika wanaoongoza ni Kenya waliokuja 93,488, wakifuatiwa na Burundi (47,418), Rwanda (26,899), Zambia(25, 372) na Uganda waliokuja 20,727.
Masolwa amesema kuwa mwaka huu wanatarajia kuingiza mapato zaidi ya mwaka 2022 kutokana na idadi ya watalii kuongezeka iliyotokana na uhamasishaji uliofanywa na Rais Samia Suluhu kupitia filamu yake ya ‘The Royal tour’ baada ya nchi kukumbwa na janga la uviko -19 mwaka 2019.
“Mwaka 2022 nchi ilifanikiwa kupata mapato yaliyotokana na utalii kiasi cha dola za Marekani million 2,527.8 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 1,310.3 ya mwaka 2021 hivyo mwaka huu tunatarajia yataongeza zaidi”amesema .
Amesema mapato hayo ya mwaka 2022 yalitokana na watalii 1,454,920 huku walioingia nchini mwaka 2021 ni 922,692.
“Idadi ya watalii wengi wanaokuja nchini ni kwa ajili ya mapumziko, wakifurahia zaidi sehemu za wanyama porina fukwe za bahari”