Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA Geofrey Tengeneza (katikati) akitoa maelezo mafupi kwa Mkurugenzi wa Bajeti, Mipango na Miliki wa NIDA Deusdedith Buberwa ya namna NIDA inavyotoa huduma kwa wananchi katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa Mbeya, Kushoto ni Afisa Usajili wa Mkoa wa Mbeya Alavuya Ntalima
Geofrey Tengeneza, Msemaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) akiagana na Masache Kasaka Mbunge wa Jimbo la Lupa, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wakati alipotembelea banda la KIDS katika Maonesho ya Nanenane, katika Viwanja vya John Mwakangale, Mkoani Mbeya.
Afisa Usajili wa Mkoa wa Mbeya Alavuya Ntalima akitoa maelezo kwa wananchi mbalimbali waliotembelea katika banda la NIDA kwenye maonesho ya Nanenane jijini Mbeya.
Geofrey Tengeneza, Msemaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) akitoa maelezo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea katika banda hilo.
………………………..
NA JOHN BUKUKU, MBEYA.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi kujisajili kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kupata huduma ya vitambulisho jambo ambalo ni rafiki kwao katika kupunguza msongamano wa watu katika ofisi za NIDA katika Mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima Nanenane kwenye Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha NIDA, Bw. Geofrey Tengeneza, amesema kuwa kuna mfumo mpya wa kujisajili katika mtandao (online) ambao unampa fursa mtanzania kutuma maombi na kukamilisha usajili kwa asilimia 75.
“Naomba watanzania wawe makini katika kujisajili kwa njia ya mtandao kwa kufata taratibu zote kadri mfumo utakavyokuwa unaelekeza” amesema Bw. Tengeneza.
Bw. Tengeneza amesema kuwa baada ya kumaliza kujaza taarifa muhimu katika mtandao, mfumo utakupa fomu ambayo utakwenda nayo serikali za mtaa kwa ajili ya kupiga mhuri.
Amefafanua kuwa baada ya hapo utakwenda katika Ofisi za NIDA kwa ajili ya kukamilisha asilimia 25 zilizobaki kwa ajili ya kupata kitambulisho cha Taifa.
Bw. Tengeneza amebainisha kuwa mpaka sasa tayari wametoa namba ya utambulisho wa Taifa kwa watu zaidi ya milioni 20 pamoja na vitambulisho vya Taifa zaidi ya milioni 13.
“Tunaendelea kutoa vitambulisho vya Taifa, tunaomba watu wote raia wa Tanzania wenye umria kuanzia miaka 18 wajisajili NIDA kwa ajili ya kupata Kitambulisho” amesema Bw. Tengeneza.
Amewataka vijana kujitokeza kujisajili na kuacha tabia ya kwenda ofisi za NIDA pale wanapokuwa na uhitaji wa matumizi ya namba ya NIDA.
Afisa Usajili Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoa wa Mbeya Bi. Lavua Maico, amesema kuwa katika maonesho ya Nanenane mwitikio ni mkubwa kwa wananchi kujitokeza kujisajili kwa ajili ya kupata Kitambulisho cha Taifa.
Amesema kuwa changamoto iliyopo baadhi ya watu wamekuwa na hofu ya kutumia mfumo mpya wa kujisajili kwa njia ya mtandao kutokana bado hawajazoe mfumo huo.
“Tunashukuru kila siku watu wengi wanakuja katika banda letu la NIDA, tunaomba tuendeleaa kujisajili kwa kufata utaratibu” amesema Bi. Maico.
Hata hivyo baadhi ya wananchi waliotembelea Banda ya NIDA Bi. Aisha Haudi pamoja na Nasoro Taitus, wameishuku NIDA kwa kuboresho utendaji wa kazi zao, kwani kwa sasa wanapata huduma kwa wakati tofauti na awali.