Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasikiliza vijana wanaoshiriki katika Programu ya Kilimo ya Jenga Kesho Iliobora (BBT) Kituo cha Bihawana mkoani Dodoma wakati akitembelea mabanda ya mbalimbali alipowasili kufungua Kongamano la Vijana linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Tarehe 07 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasikiliza vijana waliojiajiri kupitia tehama wa Dodoma Data Tech walionufaika na mkopo wa asilimia 4 kwa vijana kupitia Halmashauri wakati akitembelea mabanda ya mbalimbali alipowasili kufungua Kongamano la Vijana linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Tarehe 07 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi, watoa mada pamoja na vijana mbalimbali wakati akifungua Kongamano la Vijana linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Tarehe 07 Agosti 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya vijana mara baada ya kufungua Kongamano la Vijana linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Wengine katika picha kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara Anamringi Macha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Naibu Waziri Tamisemi Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi, Mbunge wa Kilosa na mtoa mada wa Kongamano hilo Prof. Palamagamba Kabudi pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ally Gugu.
……..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa vijana hapa nchini kujiepusha na matendo yote yasioendana na maadili ya taifa ili waweze kuaminika katika taasisi za kifedha, katika uongozi pamoja na kuwa raia wema.
Makamu wa Rais ametoa wito huo leo Agosti 07 2023 wakati akifungua Kongamano la Vijana la Mkoa wa Dodoma linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. Amesema maadili miongoni mwa vijana wengi yameporomoka ikiwemo kukosa uadilifu na hivyo kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, unyang’anyi, mapenzi ya jinsia moja, rushwa na utapeli.
Amesisitiza vijana wanapaswa kutambua uadilifu ni mtaji wa kuaminiwa na kufanikiwa hivyo ametoa rai kwa kongamano hilo kujadili kwa kina nafasi na wajibu wa wazazi, walezi, viongozi wa dini, kimila, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vijana wenyewe katika kujenga na kutunza maadili ya vijana wa Kitanzania.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa maagizo mbalimbali kwa Halmashauri hapa nchini ili kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uzalishaji mali kwa vijana ikiwemo kuanzisha kongani zinazoendana na fursa zilizopo kwenye maeneo, kuwaunganisha vijana na fursa za mitaji, kuhamasisha na kusimamia urasimishaji wa vikundi vya vijana ili viweze kutambulika. Maagizo mengine ni pamoja na kutengeneza kanzidata ya vijana na ujuzi au taaluma zao ili kuweza kuwaunganisha na fursa mbalimbali zinazojitokeza, kuhamasisha na kuwezesha vijana kuunda klabu za mazingira na kuunganisha vijana katika uzalishaji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kitaasisi zitakazosaidia kutoa ufumbuzi wa changamoto zao.
Makamu wa Rais amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira njema ya kuona vijana wa Tanzania wanaendelezwa na wanawezeshwa kushiriki katika ujenzi wa Taifa.
Amesema Kutokana na dhamira hiyo serikali imeendelea kuwawezesha vijana ili kujiari, kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia katika pato la Taifa. Ameongeza kwamba katika mwaka 2022/2023, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.88 kwa ajili ya kuwezesha miradi 85 ya vijana katika sekta za kilimo, viwanda na biashara katika halmashauri 28.
Aidha amesema Serikali ilitoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana 2,497 pamoja na kukamilisha kazi ya kuboresha Mwongozo wa Utoaji mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambapo kwa sasa unatoa mikopo kwa vijana walio katika vikundi, mtu mmoja mmoja na Kampuni.
Makamu wa Rais ametoa rai kwa vijana kujitokeza na kushiriki katika juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya maendeleo endelevu. Pia amewataka kutumia fursa zitokanazo na uhifadhi wa mazingira kama vile kuanzisha na kuendesha kampuni za ukusanyaji na uzoaji taka, uzalishaji wa funza kutokana na taka kwa ajili ya chakula cha kuku na samaki, biashara ya kaboni, uanzishaji wa vitalu na kufanya biashara ya miche ya miti na ufugaji wa nyuki.
Makamu wa Rais amesema Kongamano hilo linapaswa kufanyika katika Mikoa yote nchini ili kuwawezesha vijana kutambua fursa na kutafuta namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema mara baada ya kupitia upya utaratibu wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kutoka katika Halmashauri nchini, serikali inatarajia kuanzisha mfumo wa kielekroniki wa uombaji wa mikopo hiyo ambapo itatoa nafasi pia kwa mtu mmoja mmoja mwenye wazo zuri na lenye tija kuweza kupata mkopo pasipo kuwa na kikundi.
Awali akitoa taarifa kuhusu Kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema uwepo wa idadi kubwa ya vijana katika mkoa huo umepelekea kufanyika kwa kongamano hilo ili kuwakutanisha vijana hao na kuwaeleza mipango ya serikali na fursa zilizopo kwaajili ya kupata ajira na kujiajiri. Pia amesema kusanyiko hilo limelenga kutambua changamoto zinazowakabili vijana na kupata suluhu ya pamoja.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kwamba baada ya kongamano hilo wanatarajia kupata maazimio ya namna ya kukabiliana na ukosefu wa ajira pamoja na maadili kwa vijana. Amesema kongamano hilo litasaidia katika kukamilisha mpango mkakati wa vijana kwa mkoa Dodoma unaotarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2023.