Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewangoza Watanzania kushudia burudani ya soka kwenye mechi ya kimataifa ya kilele cha Wiki ya Simba dhiodi ya timu ya Power Dynamo ya Zambia ambapo hadi kipenga cha mwisho Simba imeshinda 2-0.
Akihutubia maelfu ya mashabiki wa timu ya Simba na watanzania waliofurika Uwanjani hapo Agosti 6, 2023 na waliofuatilia mchezo huo kupitia runinga, Rais Dkt. Samia ameipongeza timu ya Simba kwa siku kubwa na mafanikio waliyoyapa kitaifa na kimataifa.
Rais Dkt. Samia ametumia fursa hiyo kuzipongeza timu za Soka za Walemavu Tembo Warriors na timu ya Wasichana ya Serengeti Girls kwa mafanikio waliypoyapata kwa kufika hatua ya robo fainali katika mashindano ya dunia na kuongeza kuwa hivi karibuni timu ya taifa ya Wasichana U-18 kwa kutwaa ubingwa wa CECAFA 2023 kwa kuifunga Uganda 1-0.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania, Kenya na Uganda zimejipanga kuwa wenyeji wa AFCON 2027 na kusisitiza kuwa kinachosubiriwa ni ridhaa kuandaa mashindano hayo kwa kuwa ukaguzi tayari umeenda vizuri na nchi zote tatu zipo tayari kuandaa mashindano hayo.
“Serikali imejidhatiti, nia na uwezo tunao kwa kushirikiana na majirani zetu kuandaa AFCON 2027, ukaguzi wa hivi karibuni umeashiria mambo mazuri” amesema Rais Dkt. Samia.
Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali itajenga viwanja viwili vipya vya mpira katika majiji ya Arusha na Dodoma ambavyo vyote vitakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 kila kimoja.
Ametoa wito kwa wananchi na mashabiki kuendelea kutunza miundombinu viwanja vya michezo vyote nchini ili viendelee kutumika katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Akizungumza kabla ya Mgeni Rasmi kukaribishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Albert Cahalamila, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi chana amesema Rais Dkt. Samia amekuwa kinara na chachu ya kuendeleza michezo nchini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Mussa Azan Zungu, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu pamoja na viongozi wengine wa Serikali.