Na.Mwaandishi Wetu,Mwanza
Timu ya Yanga imejiweka katika mazingira magumu ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 na Pyramids FC kutoka Misri mchezo uliopigwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Wageni walikuwa wa kwanza kuandika bao kupitia kwa kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso ,Eric Traory dakika ya 42 baada ya kuachia shuti ndani ya box na kumuacha Shikalo hana la kufanya.
Hadi zikwenda mapumziko timu ya Kizazi kipya toka Misri ilikuwa mbele kwa kuongoza bao moja kwa bila.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko hata hivyo wageni walinufaika na mabadiliko hayo dakika ya 62 Nahodha wa Pyramids FC ,Abdallah Saied alifunga bao la pili.
Hata hivyo Yanga walipata bao la kuvutia machozi dakika ya 88 likifungwa na Nahodha Papy Tshishimbi na mnamo dakika ya 90 Yanga walipata pigo kwa beki wao kisiki Kelvin Yondani kuonyeshwa kadi Nyekundu.
Kwa matokeo hayo timu Pyramids FC imejiweka katika mazingira ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza wakiwa na mabao mawili ya ugenini hivyo Yanga wanatakiwa kwenda kushinda jumla ya mabao 2-0 ili waweze kupindua matokeo.