Mkuu wa mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka akipokea zawadi ya pochi ya kuhifadhia noti kutoka kwa Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania BoT Bi. Vick Msina wakati alipotembelea kwenye banda la Benki hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka akizungumza na Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania BoT Bi. Vick Msina wakati alipotembelea kwenye banda la Benki hiyo katika katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Mh. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi katika banda la Benki Kuu ya Tanzania BoT wakati alipotembelea kwenye banda hilo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. kulia ni Meneja Uhusiano na Itifaki Benki Kuu ya Tanzania BoT Bi. Vick Msina.
……………………………
NA JOHN BUKUKU, MBEYA
Watanzania wametakiwa kununua hati fungani Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na kuwasehemu salama ya kufanya uwekezaji na kuleta tija na kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka, amewataka wananchi wote kutembelea Banda la BoT kwa ajili ya kupata elimu kuhusu hati fungani.
Mhe. Mtaka amesema kuwa wastaafu wengi wamekuwa katika wakati mgumu baada ya kupokea fedha zao na kujikuta wanafanya biashara ambayo haina tija katika maendeleo ya maisha yao.
“Wananchi tutembelee banda la BOT kwa ajili ya kujifunza vitu vingi vyenye kuleta maendeleo ya uchumi pamoja na kufanya uwekezaji” amesema Mhe. Mtaka.
Amesema kuwa wakati umefika wa kununua hati fungani kwani ni eneo ambalo unakwenda kuweka fedha ambayo inaweza kuwa dhamana wakati unataka kukopa.
“Tufuatilie minada ya hati fungani, tushiriki katika minada hiyo na kununua, itawasaidia wastaafu wengi katika maisha yao” amesema Mhe. Mtaka.
Amesema kuwa hati fungani sehemu rafiki kwa watu ambao hawajawahi kufanya biashara katika ujana wao hasa wafanyakazi wa serikalini waliostaafu na wanaokaribia kistaafu.
Amesema kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakirudi nyuma kutokana na kufanya biashara ambayo hana uzoefu nayo na kujikuta anafilisika.
“Sekta binafsi wakubwa na wadogo sasa ni wakati sahihi wa kununua hati fungani, tupunguze walimu wengi, washauri baada ya kupokea fedha za kustaafu” amesema Mhe. Mtaka.
Hata hivyo ameipongeza BoT kutokana miaka yote wamekuwa karibu na wananchi katika kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya fedha na uchumi.