Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma Agosti 3, 2023 amehudhuria maonesho ya kimataifa ya Michezo ya Havana, yanayofanyika nchini Cuba na kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Akiwa kwenye maonesho hayo Mhe. Mwinjuma ametembelea moja ya banda la washiriki kutoka Cuba na kujionea teknolojia inayotumika kugundua magonjwa au kasoro ambazo zinaweza kuhatarisha maisha ya mwanamichezo mapema kabla hazijajitokeza dhahiri kwenye mwili wake.
Baada ya kujionea shughuli mbalimbali kwenye maonesho hayo Mhe. Mwinjuma amesema kuna umuhimu kwa Tanzania kutumia fursa hizo kujitangaza ili kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye michezo kwa wawekezaji wa ndani na nje watakaosaidia kuinua sekta ya michezo kwenye kila nyanja.
“Kuna Umuhimu wa kufungua mijadala ya uwekezaji mkubwa kwenye michezo ya aina zote kwani wenzetu wako mbali sana kwenye michezo, tunatakiwa kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenye kila eneo la michezo ili kuzipa timu zetu uwezo zaidi wa kifedha utakaowezesha pamoja na mambo mengi mengine matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija michezoni” amesema Mhe. Mwinjuma.