Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa Wilayani Hai kwenye ukaguzi wa miundombinu ya elimu inayojengwa kupitia mradi wa BOOST katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B”.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mroma mara baada ya kukagua miundombinu ya elimu katika shule hiyo kongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akielekea kukagua miundombinu ya elimu katika mojawapo ya Shule kongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akiwasili kukagua miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Kyuu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa akitoa taarifa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya elimu kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi, mara baada ya Naibu Waziri huyo kuwasili katika Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Hai Mhe. Saasisha Mafuwe
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.
…….
Na James Mwanamyoto (OR-TAMISEMI).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Bw. Dionis Myinga kumlipa fundi aliyepewa kandarasi ya kujenga miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa na jengo la utawala katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B” kupitia mradi wa BOOST ili akamilishe ujenzi kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, akiwa Wilayani Hai wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Shule ya Msingi Mlima Shabaha “B” mara baada ya kubaini kasi ndogo ya ujenzi iliyosababishwa na Halmashauri kutomlipa fundi madai ya fedha zake.
Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai kulipa uzito suala la usimamizi na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya elimu, kwani Serikali imepeleka fedha nyingi ili ikamilike kwa wakati na hatimaye wanafunzi wanufaike kwa kupata elimu bora.
“Fedha hizi zimeletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwawezesha mafundi kukamilisha jukumu la ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa manufaa ya taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amewata watendaji Serikalini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa uzalendo kama ambavyo Mheshimiwa Rais anavyopambana kutafuta fedha ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Hai Mhe. Saasisha Mafuwe amesema kumekuwa na changamoto ya mafundi kutolipwa kwa wakati licha ya Serikali kuwasilisha fedha katika Halmashuri ya Hai hivyo ameutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kutekeleza maelekezo ya Mhe. Ndejembi ili wananchi wanufaike na miundombinu ya elimu inayojengwa.
Sanjari na hilo, Mhe. Mafuwe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Hai ili kujenga miundombinu ya elimu na barabara.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Amiri Mkalipa amesema kuwa amepokea maelekezo ya Mhe. Ndejembi na kuongeza kuwa yeye pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama watahakikisha ujenzi wa miundombinu ya elimu unatekelezwa usiku na mchana ili Halmashauri ya Hai isiwe ni kikwazo cha jitihada za Serikali kuboresha elimu nchini.