Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya habari katika kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 3/8/2023 Jijini Dar es Salaam kuhusu utendaji wa Shirika hilo.
Watendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakisikiliza maswali na mapendekezo kutoka kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari katika kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 3/8/2023 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari wakiuliza maswali mbalimbali Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah kuhusu utendaji wa Shirika hilo katika kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 3/8/2023 Jijini Dar es Salaam.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi baada ya kupata faida ya shilingi bilioni 92.9 pamoja na kulipa kodi mbalimbali serikalini shilingi bilioni 32.4 kwa mwaka 2022/2023.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya habari katika kikao kazi kilichofanyika leo tarehe 3/8/2023 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah, amesema kuwa wataendelea kutekeleza maagizo ya Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Nchechu katika kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanatekeleza majukumu kwa ufanisi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Bw. Abdallah amesema kuwa mpaka sasa NHC wamefanikiwa kujenga Nyumba 24,000 na bado wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miji kwa kuvunja majengo ya zamani na kujenga mpya ikiwemo ya makazi pamoja na biashara ili kukizi mahitaji ya nyumba nchini.
“Tunatekeleza miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya ubia pamoja na miradi ya nyumba za gharama nafuu kwa kuweka mpango wa muda mrefu kila wilaya kulingana na mahitaji” amesema Bw.Abdallah.
Bw. Abdallah amebainisha kuwa katika mwaka 2022/23 NHC inaendelea utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ya ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Madini, Mifugo na Uvuvi, Viwanda na Biashara pamoja na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Amesema kuwa miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni pamoja na mradi wa Samia Housing Scheme ambao utakuwa na nyumba 5,000.
“Mradi huu utakuwa na nyumba za kuuza na kupangisha, unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya Rais Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani na tunatamani watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo” amesema Bw. Abdallah.
Amefafanua kuwa asilimia 50 ya nyumba katika mradi wa Samia Housing Scheme zitajengwa Dar es Salaam, huku akieleza kuwa tayari nyumba 560 zimeanza kujengwa mwezi Septemba 2022 eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa mradi huo utagharimu shilingi bilioni 466 sawa na dola za kimarekani milioni 200.
Bw. Abdallah amesema kuwa miradi mingine inayotekeleza ni Morocco Square ambao unagharimu shilingi bilioni 137 na tayari umekamilika asilimia 97.
“NHC inatekeleza majukumu mengi ikiwemo usanifu na usimamizi wa miradi ya ujenzi, utekelezaji wa sera ya ubia iliyoanzishwa mwaka 1993 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1998, 2006 na 2022 ikiwa na lengo la kuongeza na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa ushirikiano kati ya Shirika na Sekta binafsi” amesema Bw. Abdallah.
Hata hivyo amesema kuwa mpango wa matengenezo wa majengo kwa mwaka 2023/24 unalenga kufikia majengo ya zamani 101 yaliyopo katika mikoa 15 ambako NHC ina ofisi zake.
Amesema kuwa bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha shilingi bilioni 7,152, 787, 731.72.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bi. Liliani Timbuka, amesema kuwa wataendelea kufanya kazi na NHC kwa ukaribu ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.
Hata hivyo ametoa wito kwa NHC kutenga muda kwa ajili ya kuendelea kuzungumza na wahariri wa vyombo habari nchini ili waweze kujua mengi kwa ajili ya kuhabarisha umma kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.