Katibu Mkuu, sWizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amepongeza kazi inayofanywa na Shirika la Marekani la Maendeleo (USAID) kupitia mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira (MUM) kwa kuongeza na kuimarisha wigo wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Mhandisi Kemikimba amesema hayo mjini Morogoro wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa Sekta ya Maji katika kuangalia mafanikio ya utekelezaji na mipango ya MUM.
“Mradi huu ni mfano bora kwa wadau wetu wengine katika kufanya kazi na serikali katika eneo la usafi wa mazingira katika miji midogo katika kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.” Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Kemikimba amesema
Amesema miongoni mwa kazi zinazotekelezwa na za kupigiwa mfano ni kuongeza upatikanaji wa huduma endelevu za maji zinazoendeshwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira Mijini, pia kuongeza upatikanaji wa fedha za kugharamia huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Ameongeza kuwa kazi jingine ni kuimarisha bodi za mabonde ya maji na jumuiya za watumia maji ili kuziwezesha kusimamia rasilimali za maji.
Mhandisi Kemikimba amepongeza kujumuishwa kwa suala la anuai za jamii, vijana na sekta binafsi katika utekelezaji wa kazi. Aidha, mpango wa kujengewa uwezo kwa wahitimu wa wahandisi 70 ni jambo kubwa na kusisitiza wote ni muhimu katika kuimarisha masuala ya huduma ya maji katika jamii.
MUM inafanya kazi katika mikoa minne kwa wilaya 10 na mabonde ya maji manne ambayo ni: Morogoro (wilaya ya Kilombero na Kilosa), Iringa (wilaya ya Iringa DC, Kilolo, na Mufindi), Njombe (wilaya ya Ludewa na Makete) na Rukwa (wilaya ya Kalambo, Nkasi na Sumbawanga). Mabonde ni Bonde la Maji la Ziwa Nyasa, Bonde la Ziwa Rukwa, Bonde la Rufiji na Bonde la Ziwa Tanganyika